MRADI WA CHUMA WA MAGANGA MATITU KUTEKELEZWA HIVI KARIBUNI KWA USHIRIKIANO WA SERIKALI NA MWEKEZAJI

Serikali imeeleza dhamira yake ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa Chuma wa Maganga Matitu kwa haraka, kwa kushirikiana na mwekezaji wa kimataifa, ili kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inatumika kwa manufaa ya taifa. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, bungeni jijini Dodoma.

Dkt. Jafo alieleza kuwa kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Serikali imesaini Mkataba wa Ubia na kampuni ya Fujian Hexingwang Industry (Tanzania) Co. Ltd mwezi Agosti 2024 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Uwekezaji huo mkubwa unakadiriwa kugharimu dola za Marekani milioni 77.45 na unatarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka 25. Kukamilika kwa mradi huu kutaiweka Tanzania katika nafasi ya nne barani Afrika kwa uzalishaji wa chuma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri, hatua zote muhimu za maandalizi ya mradi huo zimekamilika, ikiwemo upembuzi yakinifu ambao umebainisha uwepo wa tani milioni 100 za mashapo ya chuma (iron ore) zenye kiwango cha chuma cha asilimia 44.6, Titanium Oxide kwa asilimia 11.2 na Vanadium Pentoxide kwa asilimia 0.41. Mradi unatarajiwa kuzalisha tani milioni 1.0 za chuma ghafi kwa mwaka, tani 100,000 za titanium concentrate na tani 483,000 za mabaki ya madini (tailings) kila mwaka.

Kufikia Machi 2025, Serikali kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina, NDC na mwekezaji, watakuwa wamekamilisha usajili wa Kampuni ya Ubia iitwayo Maganga Matitu Minerals Corporation Limited (MMCL) kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa mradi huo.

Katika hotuba yake, Dkt. Jafo pia alisisitiza kuwa pamoja na mradi wa chuma, Serikali itaendelea kuhamasisha ujenzi na upanuzi wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na uzalishaji wa bidhaa muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa, ikiwemo saruji, mbolea, magari, sukari, mabati na vioo

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *