NAIBU KATIBU MKUU VIWANDA AFANYA ZIARA KIWANDA CHA TBPL

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera amefanya ziara ya kikazi kwenye kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaiolojia – Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Wakati wa ziara yake hiyo, Dkt. Serera amepokelewa na mwenyeji wake Dkt. Nicolaus Shombe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), ambao ndio wasimamizi wa kiwanda cha TBPL kwa niaba ya Serikali.

Dkt. Shombe alimueleza Naibu Katibu Mkuu kuwa TBPL inazalisha bidhaa za kibaiolojia aina mbili, zisizo na kemikali sumu kwa mazingira na viumbe hai. Aina ya kwanza ikiwa ni ya kupambana na mazalia ya mbu na aina ya pili ni ya kupambana na wadudu dhurifu kwenye mazao kama pamba, korosho, mahindi na mbogamboga. “Mwaka huu tunalenga kuteka soko la viuatilifu vya kuangamiza wadudu dhurifu kwenye mazao visivyo na sumu,” alieleza Dkt. Shombe akigusia namna kiwanda hicho kilivyo na manufaa kwa Watanzania kwa kujali afya zao.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera aliitaka Bodi ya TBPL, Menejimenti na Wafanyakazi kufanya kazi kwa weledi bila kuchoka na kusisitiza kuwa kiwanda hicho kimejengwa kwa fedha za Watanzania hivyo lazima kiwanufaishe.

Aliendelea kueleza kuwa anataka kiwanda hicho kiwe cha mfano mkoani Pwani kwani ni miongoni mwa viwanda vinavyo milikiwa na Serikali ndani ya mkoa huo na anatamani kuona malengo waliyo jiwekea yakifikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *