MENU

NDC KUISAIDIA UGANDA KUANGAMIZA MAZALIA YA MBU

Ujumbe kutoka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), ukiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Viwanda vya Kuongeza Thamani (DSV), Esther Mwaigomole umefanya mazungumzo ya kibiashara na Mwakilishi wa Balozi wa Uganda, Mwambata Jeshi, Brigedia. Ronald Bigirwa, mazungumzo yaliyolenga kuuza bidhaa za kibaiolojia za kuangamiza mazalia ya mbu na za kuangamiza wadudu dhurifu kwenye mazao. Kikao kilichofanyika Ubalozi wa Uganda, jijini Dar es Salaam.

“Kwa kuanza tutatoa lita elfu moja za viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu,” alieleza Esther Mwaigomole na kumkaribisha Balozi wa Uganda nchini Tanzania kutembelea kiwanda kinacho zalisha bidhaa hizo, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kilichopo Kibaha – Pwani, kiwanda kinacho milikiwa na NDC.

Nae Mwambata Jeshi, Brigedia. Ronald Bigirwa, alifurahi kuelezwa habari hiyo njema na kuahidi kulishughulikia suala hilo kwa uharaka. “Kwa niaba ya Serikali ya Uganda niwashukuru kwa ujio wenu na nia yenu ya kufanya biashara na nchi yetu,” alieleza Brigedia Bigirwa huku akisisitiza huu ni ushirikiano mwema uliopo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Aliendelea kueleza kuwa Uganda ni nchi yenye rutuba na wananchi wengi wanajishughulisha na kilimo, hivyo dawa ya kuangamiza wadudu dhurifu kwenye mazao itapendwa na wengi, ni nafasi ya NDC kuchangamkia fursa hiyo.

Ziara hii ya NDC inakuja miezi michache baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Uganda, Mhe. Jessica Alupo juu ya umuhimu wa kutumia viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu vinavyo zalishwa na kiwanda cha TBPL.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *