NDC NA TaFF WAASISI USHIRIKIANO MPYA KWA MAENDELEO ENDELEVU YA ZAO LA MPIRA

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kushirikiana na Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) wametia saini mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji wa mradi wa ukuzaji wa zao la mpira kwa njia endelevu. Hafla hiyo muhimu imefanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu kutoka pande zote mbili, ikiwemo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Dkt. Yohana Mtoni pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa TaFF, Dkt. Tuli Salum Msuya.

Akizungumza wakati wa tukio hilo Dkt. Yohana Mtoni alisema kuwa ushirikiano kati ya NDC na TaFF ni ushuhuda wa dhamira ya Serikali kupitia taasisi zake kuhakikisha kuwa sekta ya viwanda inajengwa juu ya msingi imara wa matumizi sahihi ya rasilimali asilia. Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huu utawezesha uzalishaji wa malighafi muhimu ya mpira kwa matumizi ya viwandani, hatua ambayo itapunguza utegemezi wa bidhaa za mpira kutoka nje ya nchi na hivyo kuiwezesha serikali kuokoa fedha za kigeni sambamba na kuongeza mapato yake.

Kwa upande wake, Dkt. Tuli Salum Msuya alieleza kuwa TaFF imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa misitu ya Tanzania inahifadhiwa na kuendelezwa kwa tija. Alisisitiza kuwa mradi huu si tu unaongeza thamani ya zao la mpira, bali pia ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya kitaifa ya kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa njia ya vitendo. Aidha, alibainisha kuwa zao la mpira linaweza kuwa kichocheo muhimu cha uchumi wa kijani kwa Tanzania endapo litasimamiwa kwa njia endelevu.

Ushirikiano huu wa kimkakati unalenga kuimarisha mchango wa zao la mpira katika maendeleo ya viwanda, uhifadhi wa mazingira na kuinua kipato cha wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya mashamba ya mpira.  Kupitia mradi huu, wananchi watanufaika na ajira zinazotokana na shughuli za uzalishaji, huku pia wakipata nishati mbadala ya kuni kwa njia endelevu. Kwa mujibu wa mkataba huu, TaFF imekubali kufadhili mradi huo kwa gharama ya shilingi milioni mia nne na mbili (402,000,000/=), fedha ambazo zitatumika kutekeleza mradi huo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mradi huu pia unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa kiwango cha kimataifa kwa kusaidia kuhifadhi mazingira, kupunguza hewa ukaa, na kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan yale yanayohusu mazingira, nishati safi, ajira zenye staha na viwanda vya ubunifu. Kupitia utekelezaji wake, NDC na TaFF wanadhihirisha dhamira ya kweli ya kushirikiana katika kutafuta suluhu za changamoto zinazolikabili taifa kwa kutumia njia za ubunifu na zinazozingatia mazingira.

Kwa mafanikio ya mradi huu, NDC imejipanga kuhakikisha kuwa kila hatua ya utekelezaji inazingatia misingi ya uwajibikaji, ushirikishwaji wa wadau, matumizi sahihi ya fedha na usimamizi wa kimkakati. Hii ni hatua nyingine muhimu katika kutimiza dira ya NDC ya kuwa chombo mahiri cha serikali katika kukuza uchumi kupitia miradi ya kimkakati yenye tija kwa taifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *