NDC yaeleza mafanikio na mwelekeo wa miradi ya kimkakati nchini.

 

Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) limeeleza hatua kubwa iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, likisisitiza mchango wake katika kukuza uchumi wa Tanzania na kuifanya nchi kufikia uchumi wa kati wa viwanda.

Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Radit One, Mkurugenzi wa Viwanda wa NDC, Dkt. Mtoni, amesema kuwa shirika hilo lilianzishwa mwaka 1948 likiwa na jukumu la kuanzisha, kuendeleza na kusimamia miradi ya kimkakati kwa manufaa ya taifa.

Amesema tangu kuanzishwa kwake, NDC imekuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya viwanda nchini, ambapo imeanzisha viwanda na mashirika mbalimbali ikiwemo Tanzania Breweries (TBL), Tanzania Cigarette Company (TCC), Tanzania Oxygen pamoja na Shirika la Madini (STAMICO).

Miradi ya kimkakati ya chuma na makaa ya mawe

Dkt. Mtoni ameutaja mradi wa chuma wa Liganga na makaa ya mawe wa Mchuchuma kuwa ni miongoni mwa miradi mikubwa yenye mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

Amesema Tanzania kwa sasa hutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza chuma kutoka nje, hivyo utekelezaji wa mradi huo utasaidia kupunguza gharama hizo huku ukichochea maendeleo ya miundombinu kama ujenzi wa reli, madaraja na majengo.

“Mradi huu utazalisha ajira zaidi ya laki sita, pamoja na ajira za muda zipatazo elfu ishirini, na pia kuzalisha umeme wa megawati 600 ambapo 350 zitaingizwa kwenye gridi ya taifa,” amesema.

Aidha, amesema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutafungua fursa za kiuchumi ikiwemo ujenzi wa reli kutoka Liganga hadi Mtwara na kuchochea maendeleo ya maeneo husika.

Mradi wa magadi soda Arusha

Kwa upande wa mradi wa magadi soda, Dkt. Mtoni amesema una umuhimu mkubwa kwa viwanda mbalimbali ikiwemo vya vioo, sabuni, nguo na dawa.

Amesema mradi huo unatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 3,000 na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani huku ukichochea ukuaji wa viwanda vingine.

Kufufua viwanda vilivyokufa

Akizungumzia viwanda vilivyokufa, amesema serikali kupitia NDC imeanza kuvifufua baadhi ya viwanda ikiwemo Kilimanjaro Machine Tools (KMTC), ambacho kwa sasa kinaendelea kuzalisha na kutoa ajira.

Ameongeza kuwa juhudi zinaendelea pia kufufua viwanda vingine ili kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Changamoto na hatua zilizofikiwa

Kuhusu ucheleweshaji wa baadhi ya miradi, Dkt. Mtoni amesema miradi ya kimkakati inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha na teknolojia ya hali ya juu, hali inayochukua muda mrefu kukamilika.

Amesema mradi wa Liganga na Mchuchuma unakadiriwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani bilioni 3 sawa na Trilion 7 za Kitanzania na tayari serikali imelipa fidia kwa wananchi pamoja na kukamilisha tafiti muhimu.

“Tumefikia zaidi ya asilimia 95 ya maandalizi, na sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kumpata mwekezaji na kukamilisha mikataba,” amesema.

Fursa kwa Watanzania

NDC imewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa zitakazotokana na miradi hiyo, ikiwemo ajira, biashara ndogo ndogo na huduma mbalimbali.

Aidha, imesisitiza kuwa wawekezaji wa ndani watapewa kipaumbele endapo watakuwa na uwezo wa kifedha na kitaalamu kushiriki katika miradi hiyo.

Wito kwa wananchi

Kwa upande wake, Dkt. Mtoni ametoa wito kwa wananchi kuwa na subira kwani miradi ya kimkakati ni ya muda mrefu lakini matokeo yake ni makubwa kwa taifa.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo utaibadilisha Tanzania kiuchumi na kuongeza ustawi wa wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *