NDC YAREJESHA MATUMAINI KWA WANAKIJIJI WA IKOMELA, MBOZI, MKOANI SONGWE.

Wakulima wa Kijiji cha Ikomela kilichopo Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe, kwa kushirikiana na timu ya wataalamu kutoka kiwanda cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL),kampuni tanzu ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) – pamoja na wataalamu kutoka TPHPA Mbeya, walifanya ziara maalum ya kutembelea na kufuatilia maendeleo ya shamba lililokuwa limeathiriwa na wadudu waharibifu aina ya funza weupe (white grubs).

Ziara hiyo ni sehemu ya utafiti unaoendelea unaolenga kutathmini ufanisi wa dawa za kilimo zinazozalishwa na TBPL katika kudhibiti wadudu wanaoharibu mazao mashambani. Wakati wa ufuatiliaji huo, wataalamu na wakulima walipata fursa ya kushuhudia matokeo ya matumizi ya dawa hizo baada ya kunyunyiziwa kwenye shamba lililokuwa limeathirika.

Matokeo ya awali ya utafiti huo yameonesha mafanikio makubwa, ambapo dawa zilizotumika zimefanikiwa kuangamiza kwa kiasi kikubwa wadudu hao (funza weupe) waliokuwa wakisababisha uharibifu wa mazao. Mafanikio hayo yanatoa matumaini makubwa kwa wakulima katika kupunguza hasara inayosababishwa na wadudu hao na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Aidha, ushirikiano kati ya wakulima, wataalamu wa TBPL na TPHPA Mbeya unaonesha umuhimu wa tafiti za kisayansi katika kutafuta suluhisho endelevu la changamoto zinazowakabili wakulima. Kupitia utafiti huu, inatarajiwa kuwa matumizi ya teknolojia na dawa sahihi za kilimo yataendelea kuboreshwa ili kusaidia wakulima kupata mavuno bora na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *