NDC YASHIRIKI KATIKA KAMPENI YA AFYA CHECK

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeshiriki katika kampeni maalum ya Afya Check iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, kampeni ambayo imewakutanisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kupima afya zao pamoja na kupatiwa matibabu ya magonjwa bure.

Akizungumza katika kampeni hiyo Mkurugenzi wa Fedha wa NDC, Bi. Rhobi Sattima ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mwendeshaji amebainisha kuwa Shirika limeamua kushiriki katika kampeni hiyo kama mdhamini kwa kuwa ni mdau mkubwa katika sekta ya afya ambapo NDC inamiliki kiwanda cha kupambana na mazalia ya mbu cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

“Tuliona ni fursa kwa kuwa tunaamini maendeleo bora yanapatikana endapo watu watakuwa na afya bora na sisi pia katika kujali afya za watanzania tumewekeza katika kiwanda cha kuzalisha dawa za kupambana na ugonjwa wa Malaria kikiwa ni kiwanda pekee barani Afrika” amesisitiza Bi Sattima.

Awali akizungumza, muanzilishi na Mratibu wa kampeni hii ya Afya Check Dkt. Isack Maro amebainisha kuwa nia hasa iliyowafanya kuanzisha kampeni ya Afya Check mwaka 2009 ilitokana na Watanzania wengi kushindwa kuwa na utamaduni wa kwenda kupima afya mara kwa mara hali inayopelekea wengi wao kushindwa kubaini kuwa wana magonjwa mbalimbali katika hatua za awali na hivyo kwenda hospitali ugonjwa ukiwa katika hatua za mwisho.

“Tuliamua kuja na kampeni hii baada ya kugundua kuwa Watanzania wengi wanashindwa kupima afya zao mara kwa mara ili kubaini mapema changamoto mbalimbali zinazowakabili na kupata matibabu mapema,” amebainisha Dkt. Maro.

Hii ni mara ya kwanza kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kushiriki katika kampeni ya Afya Check ambapo ushiriki wa NDC katika kampeni hii ya Afya Check ni moja kati ya mikakati iliyowekwa na Shirika katika kuhakikisha kuwa inashiriki katika matukio mbalimbali kwa lengo la kuwafikia wadau hususani wananchi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *