MENU

NDC YAVUTIA UWEKEZAJI WA DOLA MILIONI 77.45 KATIKA MRADI WA CHUMA WA MAGANGA MATITU

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeandika historia mpya kwa kusaini mkataba wa uwekezaji na kampuni ya Fujian Hexingwang, ambao unahusisha uchimbaji wa madini ya chuma. Uwekezaji huu wa kwanza wa aina yake unatarajiwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa Ludewa, mkoa wa Njombe, na kwa Taifa kwa ujumla.

Mkataba huu umesainiwa mjini Njombe mbele ya mgeni rasmi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko. Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Dkt. Biteko alisema hatua ya kusaini mkataba huu ni matokeo ya juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha rasilimali m,abalimbali zilizopo nchini mathalani za madini zinawanufaisha wananchi.

“Mheshimiwa Rais amekuwa muumini wa kuikaribisha sekta binafsi ili kusaidia katika kukuza uchumi wa nchi yetu. Kwa utekelezaji wa mradi huu pamoja na mingine, dhamira yake ni kuhakikisha chuma kinapatikana hapa nchini,” alisema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exhaud Kigahe, alisema kusainiwa kwa mkataba huu kutapelekea kufunguka kwa fursa za kiuchumi mkoani Njombe na Taifa kwa ujumla. Aliongeza kuwa mahitaji ya chuma hapa nchini ni makubwa, ambapo asilimia mia moja ya chuma kinachotumika hulazimika kuagizwa kutoka nje ya nchi.

“Uhakiki wa taarifa za mashapo uliofanyika mwaka 2020 katika mradi huu wa Maganga Matitu umeonesha uwepo wa mashapo ya chuma tani milioni 101. Utekelezaji wa mradi huu utaongeza mnyororo wa thamani utakaokuza uchumi wa viwanda na kuokoa fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza chuma kutoka nje ya nchi,” alisema Mhe. Kigahe.

Awali, akiwasilisha taarifa ya mradi huo kwa mgeni rasmi, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, alisema mkataba huo umesainiwa kufuatia majadiliano ya muda mrefu baina ya pande zote mbili. Kwa mujibu wa mkataba huo, mwekezaji atawekeza Dola za Kimarekani milioni 77.4 kama mtaji (equity) na sio mkopo. Pia, atajenga mgodi wa chuma wenye uwezo wa kuzalisha tani milioni 1 kwa mwaka na kiwanda cha kuchenjua chuma ghafi.

Makubaliano mengine ni pamoja na mwekezaji kulipa fidia kabla ya Januari 2025, ambapo Halmashauri ya Ludewa imekamilisha uthamini wa wananchi 385 watakaolipwa kiasi cha Shilingi 4,215,600,214.47. Pia, kampuni ya ubia (JVC) itaundwa na wabia watatu: NDC, Fujian Hexingwang, na Serikali. Kampuni ya ubia itaendeshwa kwa pamoja kati ya mwekezaji na Watanzania ili kujenga uwezo wa Watanzania na kuhakikisha uwazi katika uendeshaji wa kampuni.

Umiliki wa hisa katika mkataba huu utahusisha kampuni ya Fujian Hexingwang ambayo itamiliki 64% ya hisa, NDC itamiliki 20% ya hisa, na Serikali kupitia msajili wa Hazina itamiliki hisa 16% (non-dilutable free carried interest shares) kwa mujibu wa Sheria ya Madini (State Participation) Sura ya 123 na kanuni zake za mwaka 2022.

 

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *