NDC YAWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUTOKA KOREA KUWEKEZA KATIKA MIRADI YAKE

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limewaalika wawekezaji kutoka Korea kuwekeza katika miradi ya kimkakati inayosimamiwa na shirika hilo, hatua inayolenga kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda nchini.

Hayo yameelezwa leo katika semina ilichofanyika katika hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam, iliyojumuisha NDC, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Kituo cha Uwekezaji wa Kibiashara cha Korea (KOTRA), pamoja na makampuni mbalimbali ya uwekezaji. Kikao hicho, kilichoitwa “2024 Korea-Tanzania Project Plaza,” kilikuwa na lengo la kujadili fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania ambazo wawekezaji kutoka Korea wanaweza kunufaika nazo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Mhandisi Alex W. Rumanyika aliwahamasisha wawekezaji kutoka Korea kuwekeza katika miradi mbalimbali inayosimamiwa na shirika hilo, ikiwemo Mradi wa Kilimanjaro Machine Tools Company (KMTC), Mradi wa Magadi Soda wa Engaruka mkoani Arusha, Mradi wa Mang’ula Machemical and Spare Parts uliopo Mang’ula mkoani Morogoro, pamoja na kongane za Kange na TAMCO zinazomilikiwa na shirika hilo.

Mhandisi Alex alisisitiza kuwa NDC iko tayari kushirikiana na mwekezaji yeyote atakayeonyesha nia ya kuwekeza kwenye miradi yake, kwa kutoa ushirikiano wa kutosha, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya serikali kuhakikisha kuwa NDC inashirikiana na wawekezaji binafsi kwa niaba ya serikali na kujenga mazingira bora ya uwekezaji yatakayowanufaisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Awali, Balozi wa Korea nchini Tanzania, Bi. Eunju Ahn, amesema kuwa kikao hicho ni muhimu sana kwani kinachangia kuboresha mahusiano ya muda mrefu baina ya Korea na Tanzania na kutasaidia kuzifanya nchi hizi kunufaika kiuchumi kwa kuwa wafanyabiashara na wawekezaji wa Korea watapata fursa ya kufahamu nafasi za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania.

Kikao hicho kimehudhuriwa na makampuni themanini kutoka Tanzania, na makampuni arobaini kutoka Korea, ambapo kwa pamoja walijadili fursa za kiuchumi na uwekezaji zinazoweza kutumiwa na wawekezaji kutoka Korea ili kuboresha sekta ya uwekezaji nchini kwa manufaa ya pande zote mbili, Tanzania na Korea.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *