Mabalozi 7 wa nchi za Afrika zikiwemo Afrika kusini, Sudan ya Kusini, Nigeria,
Saharawi, Comoro, Msumbiji na Zambia wakiwa wameambatana na Balozi wa
Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne wametembelea kiwanda cha
kibaiolojia cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu, Tanzania
Biotech Products Limited (TBPL), cha Kibaha, Pwani na kuipongeza Serikali ya
Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa uwekezaji wenye tija na
lengo la kupambana na ugonjwa wa malaria nchini na Afrika kwa ujumla.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe
ambaye ndiye mwenyeji wa ugeni huo aliwashukuru mabalozi hao kwa ujio wao
kiwandani hapo kujifunza na kuona namna wanavyoweza kushirikiana na Serikali ya
Tanzania kupambana na ugonjwa wa malaria na kuwaeleza mchango wa kiwanda hicho
nchini na Afrika kwa ujumla.
“Kiwanda hiki kimechangia kiasi kikubwa kwenye
mapambano dhidi ya malaria tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 ambapo kiwango kilikua
14% na kushuka hadi 7%,” alieleza Dkt. Shombe.
Alikazia matarajio ya nchi ni kufika asilimia 3
ifikapo mwaka 2025 na kwa Afrika ni kufika 0% ifikapo mwaka 2030.
Kiwanda cha viuadudu kinaenda sambamba na Malengo
Endelevu hasa lengo la 5 na 6 la kupambana na vifo vya mama na mtoto pamoja na
ugonjwa wa malaria.
Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wengine, Balozi wa
Comoro nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed ameeleza kiwanda cha viuadudu ni muhimu kwa Waafrika wote ndio maana wamekitembelea na
kuhakikisha malaria ina angamizwa.
Alifafanua zaidi kwa kusema amefurahishwa na taarifa
aliyopewa kuwa viuadudu vinavyo zalishwa kiwandani hapo havina madhara kwa
mazingira na viumbe wengine bali kiluwiluwi cha mbu pekee.
“Tumehakikishiwa bidhaa hizi hazina madhara kwa
mazingira na binadamu hivyo nadhani zinafaa nchini Comoro,” ameeleza Balozi
Dkt Ahamada El Badaoui Mohamed.
Akiunga mkono hoja hiyo, Balozi wa Algeria nchini Tanzania Mhe Ahmed Djellal amesema mchango wa viuadudu utakuwa na manufaa kwao hasa ukanda wa kusini wa Algeria.
“Siku
chache zilizopita niliugua malaria, hivyo nimeelewa ugonjwa ulivyo,” ameleeza
Balozi. Kwa kuona athari za ugonjwa huo, Balozi huyo ameeleza kuwa lengo lake
kama balozi ni kuhakikisha usalama wa raia wake na kusema viuadudu hivyo
vitawafaa.
Mhe. Hamisu Umar Takamawa, Balozi wa Nigeria
nchini Tanzania ameipongeza Serikali ya Tanzania na Cuba kwa kuwezesha ujenzi
wa kiwanda cha viuadudu na kusaidia mapambano dhidi ya malaria barani Afrika.
Akizungumza kwa niaba
ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Kibaha Clemence kagaruki amesema
anakipongeza kiwanda kwa mwaliko hivyo wakitoka hapo watakuwa mabalozi wazuri
kutangaza kiwanda dhidi ya malaria.
“Nimejifunza kuwa
tunaweza tukanufaika na kiwanda hiki kwenye mapambano dhidi ya Malaria,”
ameeleza kagaruki.
Mbali na kuzalisha
viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu, Meneja wa Kiwanda hicho, Samuel Mziray
ameeleza kuwa wapo mbioni kuzalisha mbolea za kibaiolojia pamoja na viuatilifu
vya kibaiolojia ambavyo vitakuwa ni
mkombozi kwa kilimo cha Tanzania na Afrika kwa ujumla kwani havitakuwa na
kemikali dhurifu kwa mazao mbalimbali.
Amekazia kuwa majaribio tayari yameshafanyika na
matokeo ni mazuri hivyo wapo kwenye hatua za mwisho za kuanza uzalishaji wa
kibiashara ili iwe mkombozi kwa wakulima.