MENU

NDC HATUNA MSONGO WA MAWAZO

Mabalozi 7 wa nchi za Afrika zikiwemo Afrika kusini, Sudan ya Kusini, Nigeria, Saharawi, Comoro, Msumbiji na Zambia wakiwa wameambatana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne wametembelea kiwanda cha kibaiolojia cha kuzalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), cha Kibaha, Pwani na kuipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa uwekezaji wenye tija na lengo la kupambana na ugonjwa wa malaria nchini na Afrika kwa ujumla.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe ambaye ndiye mwenyeji wa ugeni huo aliwashukuru mabalozi hao kwa ujio wao kiwandani hapo kujifunza na kuona namna wanavyoweza kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupambana na ugonjwa wa malaria na kuwaeleza mchango wa kiwanda hicho nchini na Afrika kwa ujumla.

“Kiwanda hiki kimechangia kiasi kikubwa kwenye mapambano dhidi ya malaria tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 ambapo kiwango kilikua 14% na kushuka hadi 7%,” alieleza Dkt. Shombe.

Alikazia matarajio ya nchi ni kufika asilimia 3 ifikapo mwaka 2025 na kwa Afrika ni kufika 0% ifikapo mwaka 2030.

Kiwanda cha viuadudu kinaenda sambamba na Malengo Endelevu hasa lengo la 5 na 6 la kupambana na vifo vya mama na mtoto pamoja na ugonjwa wa malaria.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi wengine, Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Mhe. Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed ameeleza kiwanda cha viuadudu ni muhimu kwa Waafrika wote ndio maana wamekitembelea na kuhakikisha malaria ina angamizwa.

Alifafanua zaidi kwa kusema amefurahishwa na taarifa aliyopewa kuwa viuadudu vinavyo zalishwa kiwandani hapo havina madhara kwa mazingira na viumbe wengine bali kiluwiluwi cha mbu pekee.

“Tumehakikishiwa bidhaa hizi hazina madhara kwa mazingira na binadamu hivyo nadhani zinafaa nchini Comoro,” ameeleza Balozi Dkt Ahamada El Badaoui Mohamed.

Akiunga mkono hoja hiyo, Balozi wa Algeria nchini Tanzania Mhe Ahmed Djellal amesema mchango wa viuadudu utakuwa na manufaa kwao hasa ukanda wa kusini wa Algeria.

“Siku chache zilizopita niliugua malaria, hivyo nimeelewa ugonjwa ulivyo,” ameleeza Balozi. Kwa kuona athari za ugonjwa huo, Balozi huyo ameeleza kuwa lengo lake kama balozi ni kuhakikisha usalama wa raia wake na kusema viuadudu hivyo vitawafaa.

Mhe. Hamisu Umar Takamawa, Balozi wa Nigeria nchini Tanzania ameipongeza Serikali ya Tanzania na Cuba kwa kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha viuadudu na kusaidia mapambano dhidi ya malaria barani Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Kibaha Clemence kagaruki amesema anakipongeza kiwanda kwa mwaliko hivyo wakitoka hapo watakuwa mabalozi wazuri kutangaza kiwanda dhidi ya malaria.

“Nimejifunza kuwa tunaweza tukanufaika na kiwanda hiki kwenye mapambano dhidi ya Malaria,” ameeleza kagaruki.

Mbali na kuzalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu, Meneja wa Kiwanda hicho, Samuel Mziray ameeleza kuwa wapo mbioni kuzalisha mbolea za kibaiolojia pamoja na viuatilifu vya kibaiolojia ambavyo vitakuwa ni mkombozi kwa kilimo cha Tanzania na Afrika kwa ujumla kwani havitakuwa na kemikali dhurifu kwa mazao mbalimbali.

Amekazia kuwa majaribio tayari yameshafanyika na matokeo ni mazuri hivyo wapo kwenye hatua za mwisho za kuanza uzalishaji wa kibiashara ili iwe mkombozi kwa wakulima.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *