Mkurugenzi mwendeshaji wa shirika la Taifa Maendeleo NDC Dk Nicolaus Shombe amekishauri chuo cha elimu ya Biashara CBE kuhakikisha kinatengeneza mitaala ya kufundishia inayoendana na mazingira ya biashara yaliyopo duniani hivi sasa.
Dk Shombe ameyasema haya jijini Dar es Salaam wakati alipoalikwa kuwa mgeni maalum katika shughuli ya CEOs Breakfast tukio ambalo liliwakutanisha wakuu wa Taasisi mbalimbali hapa nchini ambao kwa pamoja kwa kushirikiana na chuo cha elimu ya biashara CBE wamejadili namna ya kukuza nguvu kazi katika soko la ajira.
Akizungumza katika kongamano hilo Dk Shombe amesema mazingira ya hivi sasa ya ufanyaji wa biashara yamebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma hali inayoweza kupelekea hata namna ya ufundishaji wa elimu ya biashara nayo kubadilika.
“Dunia ya leo mazingira ya biashara yamebadilika sana ni tofauti na miaka iliyopita zamani ukiongelea bishara unaongelea Kariakoo lakini saizi unavyoongelea biashara unaongelea ufanyaji wa biashara katika mitandao ya kijamii unakuta mtu ana duka kubwa mtandaoni Instagram kuliko hata aliye na duka mtaa wa Samora” Alibainisha Dk Shombe.
Dk Shombe aliitaka CBE kuhakikisha inakuja na mitaalam ambayo itakuwa inawaandaa wanafunzi wanaohitimu katika fani ya biashara kuweza kutumia fursa zilizopo za kukua kwa sayansi na teknolojia na hatimaye kuweza kushindana katika soko la ajira.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha elimu ya Biashara CBE Prof Edda Lwoga amesema katika kuhakikisha wanazalisha wahitimu wenye uwezo wa kupambana na soko la ajira mwaka 2022 chuo hicho kilifanya utafiti maalum kwa lengo la kujua hali ya wahitimu wa chuo hicho na kuangalia na jinsi wanavyoendana na hali halisi ya mahitaji ya soko la ajira.
Akiwasisha ripoti hiyo Profesa Lwoga amesema kuwa matokeo ya uatafiti huo yameonyesha kuwa asilimia 79.5 ya wahitimu wa chuo hicho wanaweza kujiajiri huku asilimia 59.5 ya wahitimu wameajiliwa na mashirika ya umma na binafsi wakati asilimia 20 wamejiajiri na asilimia 20.5 bado wanatafuta ajira.
“Matokeo haya yanaonyesha kuwa CBE tupo katika njia sahihi ya kuzalisha wataalam wanaohitajika katika sekta ya viwanda na biashara lakini pia tunahitaji maboreho na hii CEO Breakfast ni moja kati ya nia yetu ya kupata mrejesho ili tuweze kuboresha elimu tunayotoa na kuzalisha wataalam wanaohitajika na soko” alisisitiza Prof Lwoga
Awali Mkuu wa Chuo cha CBE Mstaafu Prof Emmanuel Mjema ambaye pia ndiye mwanzilishi wa CEO Breakfast amewashukuru washiriki walioshiriki katika tukio hilo na kwamba kufanikiwa kwake kunasaidia kwa kiwango kikubwa kwa Chuo cha elimu ya biashara kuboresha huduma zake inazozozitoa katika jamii kwa kuwa washiriki hupata muda wa kutoa maoni na mtazamo wao wa uboreshaji wa huduma za chuo hicho.
Chuo cha biashara CBE kilianzishwa mwaka 1965 ambapo kwa hivi sasa inatoa elimu kwa ngazi mbalimbali ikiwemo shahada na uzamili katika fani mbalimbali ambapo hii ni mara ya tatu kwa CEOs Breakfast kufanyika hapa nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2021 ambapo hutumika kama jukwaa la kuwakutanisha wadau wa kutoka kada mbalimbali ambao kwa kushirikiana na chuo cha elimu ya biashara CBE hujadili mambo mbalimbali yahusuyo uboreshaji wa mazingira ya kufundishia elimu ya biashara hapa nchini.