Rais wa Bunge la Cuba, Mhe. Esterban Lazo Fernandiz amefurahishwa na kupongeza uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria pamoja na kuongeza upatikanaji wa chakula kupitia uzalishaji wa viuatilifu hai visivyo na sumu.
Ameyasema hayo alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja kwenye kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaiolojia, Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) @tbpltanzania , Kibaha mkoani Pwani.
Aliongeza kuwa kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), ni kielelezo cha ushirikiano baina ya Tanzania na Cuba kwani teknolojia inayotumika hapo inapatikana nchini Cuba.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwajali Watanzania kwa kuwajengea kiwanda hicho cha kipekee barani Afrika na kutoa rai kwa Halmashauri zote zinazo chukua viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu kiwandani hapo kuhakikisha wanatumia kulingana na maelezo ya wataalam ili ziwe za manufaa kwa jamii.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Suleiman Selela ameipongeza NDC kwa kuendelea kukisimamia kiwanda hicho na amewahakikishia Serikali itaendelea kushirikiana na NDC pamoja na TBPL ili kuhakikisha kiwanda hicho kinaleta tija si tu kwa Taifa bali nje ya mipaka ya Tanzania na kuzidi kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia diplomasia tiba “health diplomacy.”
“Tumeongeza bidhaa mpya, viuatilifu hai ?T- 24), visivyo na kemikali kwa ajili ya kuangamiza wadudu dhurifu kwenye mazao,” ameeleza Dkt. Nicolaus Shombe, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, akitanabaisha kuwa lengo la kiwanda cha TBPL ni kuhakikisha kinalinda afya za Watanzania kwa kuzalisha bidhaa zisizo na kemikali.
Ameeleza kuwa shabaha namba moja ya kiwanda ni kutokomeza malaria sambamba na kuongeza tija kwenye upatikanaji wa chakula kwa kuzalisha bidhaa zisizo na kemikali kwa ajili ya mazao na sasa kiwanda kipo kwenye mchakato wa kuongeza mbolea hai.