Serikali imebainisha kuwa ipo katika hatua za mazungumzo na mwekezaji wa mradi wa uchimbaji chuma na makaa ya mawe wa Liganga na Mchuchuma ili kuanza mara moja kwa utekelezaji wa mradi huu hapa nchini.
Haya yamebainishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo mapema leo ambapo amefanya ziara ya ukaguzi wa mradi huo ziara iliyofanyika Wilayani Ludewa, Mkoani Njombe ambapo Mh. Jafo alipata fursa ya kutembelea na kuona maendeleo ya utekelezaji wa mradi huu.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mundindi Dkt. Jafo amesema kuwa utekelezaji wa Mradi huu unatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuongeza uzalishaji wa chuma na pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi huku akiwahimiza wananchi kutumia fursa ya utekelezaji mradi huu kuweza kujiinua kiuchumi kwa kuchangamkia fursa za kibiashara na ajira zitazoambatana na utekelezaji wa mradi huu.
Katika hatua nyingine Jafo amewaasa wananchi juu ya utunzaji wa amani ya nchi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu, huku aliwahimiza watendaji wa Serikali kutumia dhamana waliyopewa kama watumishi wa Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazo stahiki kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.
Kwa upande wake Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga ameonyeshwa kufurahishwa na jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo katika utekelezaji wa mradi huu amefanikiwa kuhakikisha anaboresha miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami katika wilaya hiyo pamoja na upanuzi katika sekta ya elimu pamoja na afya.
Mradi wa Liganga na Mchuchuma ni mradi mkubwa wa kimkakati wa uchimbaji wa madini ya chuma, pamoja na makaa ya mawe ulioko chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ambao utekelezaji wake utapelekea kuzalisha chuma kinachotumika viwandani kwa matumizi ya ndani na nje ya nchi.