Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Kugawa Miche 193,000 ya Mpira Bure

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) limeandika historia mpya katika kata ya Mwaya, Kilombero, mkoani Morogoro kufuatia kufanyika kwa ufunguzi maalum wa zoezi la upandaji wa miti ya mpira katika eneo la shamba la mpira la Kalunga. Tukio hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya mpango wa kugawa bure miche ya miti ya mpira 193,000 kwa wananchi wanaozunguka shamba hilo, kwa lengo la kuwashirikisha kikamilifu katika kilimo cha zao la mpira na kuinua uchumi wa kaya zao.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, ambaye aliongoza zoezi la upandaji wa miti pamoja na wanakijiji na viongozi wa Serikali wa maeneo hayo.

Katika hotuba yake, Dkt. Shombe alieleza kuwa mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa mpira nchini, kuchochea maendeleo ya viwanda vya ndani, na kufungua fursa zaidi za ajira kwa vijana na wanawake.

Aidha, alisisitiza kuwa miche hiyo imezalishwa kupitia mradi wa upandaji wa mpira unaoratibiwa na NDC kwa ufadhili wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), na kwamba ushiriki wa wananchi ni nguzo muhimu ya mafanikio ya mradi huo. Alitoa wito kwa wananchi kuitunza miche watakayopatiwa ili kuhakikisha inaleta tija iliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Viwanda vya Kuongeza Thamani, Bi. Esther Mwaigomole, alisema kuwa uwekezaji katika zao la mpira utaongeza malighafi kwa viwanda vya ndani vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali zitokanazo na mpira, hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Naye Meneja wa Mradi, Bw. Egata Makanja, alieleza hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, akibainisha kuwa maandalizi ya mashamba darasa, utoaji wa mafunzo kwa wakulima, na ufuatiliaji wa kitaalamu vitaendelea kufanyika ili kuhakikisha miti inapandwa na kustawi kwa viwango vinavyokubalika.

Viongozi wa serikali kata ya mwaya waliohudhuria hafla hiyo walionyesha furaha na matumaini makubwa, wakisema kuwa mradi huo utachochea kipato cha wananchi na kubadilisha maisha yao. Baada ya hotuba, viongozi hao walishiriki kupanda miche ya mpira kama ishara ya uzinduzi rasmi wa zoezi hilo.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *