MENU

TAARIFA YA MKURUGENZI MWENDESHAJI WA SHIRIKA LA TAIFA LA MAENDELEO (NDC) DKT. NICOLAUS SHOMBE AKIZUNGUMZA NA KUHUSU UTEKELEZAJI NA VIPAUMBELE VYA SHIRIKA KWA MWAKA 2023/2024

Ndugu Waandishi wa Habari,

1.1 Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na kutukutanisha leo hii tukiwa buheri wa afya. Nawashukuru sana pia Wanahabari wote kwa kuitikia mwito kuu. Kwa Serikali na sisi wana NDC tunaamini kuwa ninyi ni wadau muhimu sana kwani kupitia kwenu, taarifa mbalimbali zinazohusu Nchi na Shirika Taifa la Maendeleo zinawafikia umma wa Watanzania na hivyo kujenga ufahamu wa masuala ya Taasisi na pia kuwaandaa kutumia fursa na kutoa ushirikiano unaohitajika kwa maendeleo ya Watanzania. Kazi hiyo mnaifanya vema na ninawapongeza sana.

1.2 Kipekee na kwa niaba ya wafanyakazi wenzangu wa NDC, napenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mheeshimiwa Dkt. Filipo Mpango, Makamu wa Rais na Mheshimiwa Kasim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kulithamini na kuliamini Shirika la Taifa la Maendeleo likiwa ni mkono wa Serikali wa uwekezaji. Katika msingi huo, Serikali imeendelea kuliwezesha Shirika na kulipatia umuhimu stahiki katika kuendeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya kimkakati na kielelezo inayosimamiwa na NDC kwa maendeleo ya Taifa letu. Pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt.Ashatu K. Kijaji (Mb.), Waziri wa Viwanda na Biashara na Mheshimiwa Exaud S, Kigahe (Mb.), Naibu Waziri kwa kuwa chachu muhimu kiuongozi na kidira katika kuliendeleza Shirika hili. Aidha, nawashukuru Viongozi mbalimbali wa Wizara, Taasisi, Sekta Binafsi, wabia mbalimbali na umma wa Watanzania kwa kutupatia ushirikiano usio na shaka katika kuhakikisha kuwa Mipango na Mikakati ya Taasisi yetu inatekelezwa kwa umakini na tija. Kwa kufanya hivyo imewezesha na kuhakikisha kuwa Shirika linaimarika na kufanikiwa kubaki katika mstari na dira ya kuundwa kwake na hivyo kutoa mchango unaotakiwa katika maendeleo ya Taifa. Nasi tunaahidi kuendelea kujibidisha na kuboresha ushirikiano nanyi tukitambua kuwa mafanikio yetu ndiyo mafanikio yenu na sina shaka kuwa kwa hakika tunaweza.

Ndugu Wanahabari,

1.3 Leo tarehe 25/8/2023, tumeona tuwaite hapa ili tuwahabarishe kuhusu utekelezaji wa mipango na vipaumbele vya Shirika kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwa ni (mwaka mmoja na miezi kumi) tangu niteuliwe rasmi na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC). Natambua kuwa hii ni dhamana kubwa ambayo ninaithamini na ni azma yangu kuleta tofauti ya kiutendaji na matokeo ili umuhimu wa Shirika hili uendelee kudhihirika zaidi na zaidi. Aidha, nakusudia kuelezea dira na mwelekeo wa Shirika kwa muktadha wa mipango mikakati na kuzingatia maelekezo ya Serikali na hususan nikirejea maelekezo ya mamlaka katika uendeshaji wa mashirika ya umma. Tunaamini kuwa maelekezo hayo yatakoleza kasi na dhamira ya Shirika kuwa mkono wa uwekezaji ambao hatimaye kuwanufaisha Watanzania kimaisha na staha kwa uendelevu.

 1. HISTORIA YA SHIRIKA

Ndugu Wanahabari,

Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ni Shirika kongwe kuliko mashirika karibu yote ya umma nchini, likiwa limeanzishwa Mwaka 1948 likijulikana kama Colonial Development Corporation (CDC). Shirika hilo baadaye lilibadilishwa jina na kuitwa Agricultural Development Corporation (ADC) baada ya makoloni mengi kuanza kupata uhuru. Kuelekea Mwaka 1961, Shirika hilo liliunganishwa na Shirika jingine lililofanana na hilo la Mwananchi Development Corporation lililokuwa mali ya Chama cha TANU na kuunda Shirika lililojulikana kama Tanganyika Development Corporation (TDC). Kufuatia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Mwaka 1964, jina la Shirika likabadilishwa na kuwa Shirika la Taifa la Maendeleo (National Development Corporation – NDC), jina ambalo linalotumika hadi sasa. Shirika hilo ndilo linalotubebea agenda ya maendeleo ya uwekezaji wa miradi mikubwa ya kitaifa katika kipindi chote hasi sasa ambapo kumekuwepo na mabadiliko ya majukumu kulingana na mazingira ya kiuchumi na kijamii, kupitia kipindi cha Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea (Azimio la Arusha) na baadaye uchumi wa soko huria.

Ndugu Wanahabari,

Shirika likiwa ni mkono wa Serikali wa uwekezaji limekuwa likisimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi hapa nchini ambayo inagusa sekta muhimu za kilimo, viwanda, madini, nishati, miundombinu na biashara kwa lengo la kuharakisha maendeleo. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kuwafamisha baadhi ya miradi ambayo inatekelezwa na Shirika,Mafanikio pamoja na mwelekeo mzima wa Shirika katika kuunga mkono dira, sera na mipango ya Serikali katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

 1. MIRADI INAYOTEKELEZWA NA SHIRIKA

Ndugu Waandishi wa Habari,

4.1 Kihistoria Shirika la NDC ndiyo ilikuwa ni kiota cha kutotolesha viwanda nchini. Katika kipindi kirefu, NDC iliweza kuanzisha Viwanda na mashirika tanzu ambayo yamekuwa yakitoa mchango mkubwa kimapato, ajira na katika Pato la Taifa. Aidha, vingi ya viwanda vikubwa vinavyoendelea nchini hivi sasa na baadhi ya mashirika ni matokea ya kazi ya NDC. Mifano hai ni Kiwanda cha TBL, ALAF, TCC, mashirika ya STAMICO, SIDO, nk.

Ndugu Waandishi wa Habari,

4.2 Kufuatia mageuzi na mabadiliko mbalimbali yaliyofanywa, kwa sasa, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linasimamia miradi ifuatayo:

 • Miradi nane (8) ya Viwanda Mama (Basic Industrial Projects) inayojumuisha:
  • Miradi mitatu (3) ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma, Katewaka na Ngaka
  • Mradi wa Chuma wa Liganga,
  • Mradi wa Magadi-Soda wa Engaruka,
  • Kiwanda cha Kutengeneza Matairi cha Arusha,
  • Kiwanda cha Mashine cha Mang’ula, na
  • Kiwanda cha Vipuri cha Kilimanjaro (KMTC).
 • Miradi mitatu (3) ya Kuongeza Thamani (Strategic Value Addition Projects) inayojumuisha:
  • Kiwanda cha Uzalishaji wa Viuadudu cha Tanzania Biotech Products Limited – Kibaha, Pwani,
  • Bandari Kavu ya Nafaka – ETC Cargo – Mbagala Dar es Salaam, na
  • Mashamba ya Mpira ya Kalunga – Morogoro na Kihuhwi – Tanga.
 • Maeneo manne (4) ya Viwanda (Industrial Parks/Estate) yanayojumuisha:
  • Eneo la Viwanda la TAMCO – Kibaha Pwani,
  • Eneo la Viwanda la Kange – Tanga,
  • Eneo la Viwanda la KMTC – Moshi, na
  • Eneo la Viwanda la Nyanza – Mwanza.

Ndugu Waandishi wa Habari,

4.3 Kwa kuzingatia heshima, juhudi na nia ya dhati ya Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya kujenga uchumi imara usio – tegemezi, Shirika la Taifa la Maendeleo liko naye bega kwa bega likifanya kazi kwa uadilifu na ubunifu mkubwa kwa kuhakikisha kuwa kunakuweko na tija katika utendaji wake. Hivyo, ili kufanikisha maono hayo, NDC imeendelea kutekelaza miradi mbalimbali ya maendeleo na limeweza kufanikisha masuala mbalimbali kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuinua Sekta ya Viwanda na Uwekezaji nchini. Hivyo, Shirika linapenda kuwahabarisha ili pia umma wa Watanzania wayasikie na kuwakumbusha kwa rejea nafasi, umuhimu na thamani ya Shirika la Taifa la Maendeleo katika mukatadha wa kuliletea Taifa maendeleo endelevu.

 1. MAFANIKIO YA SHIRIKA

5.1 Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Shirika limefanikisha yafuatayo:

1)         Utekelezaji wa Mradi wa Kielelezo wa Liganga na Mchuchuma.

Ndugu Wanahabari,

5.2 Mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao uko Wilayani Ludewa katika Mkoa wa Njombe ulikabidhiwa kwa NDC mwaka 1996 na kuanza utekelezaji mwaka 2007 ambapo Shirika limewezesha kufanyika tafiti mbalimbali ambazo zimebainisha yafuatayo:

(a)        Tathmini ya madini – ilifanyika mwaka 2011 – 2015 na kubaini uwepo wa mashapo ya chuma kiasi cha tani 126 milioni katika eneo la kilometa za mraba 10 na makaa ya mawe tani 426 milioni kwenye eneo la kilomita za mraba 30. Utekelezaji wa mradi umepanga kuchimba chuma tani 2.9 milioni kwa mwaka na kuzalisha bidhaa za chuma (steel) tani 1 milioni kwa mwaka. Aidha chuma cha Liganga kimechanganyika na madini mengine ambayo ni Titanium na Vanadium na ambayo yana thamani kubwa kuliko chuma.

(b)        Mwekezaji – Serikali ilipata mwekezaji Sichuan Hongda mwaka 2007 kusaini mkataba 2011kwa njia shindani ambaye pia ana teknolojia ya kuchenjua chuma na madini mengine

(c)        Kufanya tathmini ya mali za wananchi watakaopisha Mradi (tathmini ya kwanza mwaka 2015 Shilingi bilioni 13.4 na pili mwaka 2018 ulifanyika uhakiki ambapo jumla ya shilingi bilioni 11.4 na uhuishaji wake kufanywa mwaka 2022/23 ambapo thamani ya fidia ni Shilingi bilioni 15.4 baaada ya uhakiki ikiwa na riba ya miaka mitano)

5.3 Mradi wa Liganga na Mchuchuma ni tofauti na miradi mingine, ni mradi unganishi kwani unatekelezwa kwa pamoja na inategemeana. Huu ni moja ya miradi ya kimkakati na kielelezo iliyobainishwa katika Dira ya Taifa 2025, Ilani ya CCM na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Hivyo, katika kutekeleza na kutambua umuhimu wa Mradi huo katika kwa uchumi wa nchi yetu, kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Shirika limefanikiwa kufanya yafuatayo:

 1. Shirika limefanikiwa kulipa fidia ya jumla ya Shilingi 15,424,364,900 kwa wananchi wanaopisha utekelezaji wa miradi ya Mchuchuma (Shilingi bilioni 5) na Liganga (Shilingi bilioni 10) ambapo jumla zilitolewa na Serikali. Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2023, jumla ya wanufaika 1,048 walilipwa fidia kati ya 1,142 sawa na asilimia 91.76. Ulipaji huo wa fidia ambao umesubiriwa na wananchi kwa miaka mingi unaifanya Serikali kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuendeleza uwekezaji kwa manufaa mapana ya Taifa.
 2. Licha ya kufanikisha ulipaji wa fidia, Shirika pia limefanikiwa kupata leseni kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa Makaa ya Mawe nje ya leseni kubwa ya Mchuchuma. Upatikanaji wa leseni hizo unaliruhusu Shirika kuanza uchimbaji wa Makaa ya Mawe ambapo Kampuni tano (5) za wazawa zinatarajia kuanza uchimbaji katika eneo la Mchuchuma ndani ya mwaka 2023/2024.

iii.        Kuanza majadiliano na mwekezaji ili kutatua changamoto za kimkataba na kuendelea na hatua za ujenzi wa Kiwanda na Migodi ya Makaa ya Mawe na Chuma cha Liganga na Mchuchuma. Majadiliano hayo yanahusisha leseni kubwa ya uchimbaji wa madini (Specail Mining Licence)

Ndugu Wanahabari

5.4 Katika kuendeleza jitihada hizo, Shirika kwa mwaka wa fedha 2023/2024, limepanga kutimiza maono ya kutekeleza Mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao kwa miaka mingi ulikuwa ikikabiliwa na mikwamo licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa uchumi wa Nchi kwa kufanya mambo yafuatayo:

 1. Kukamilisha majadiliano na mwekezaji na kusaini Mkataba wa Ubia. Majadiliano hayo yanategemea kukamilishwa ndani ya mwaka wa fedha 2023/2024 na hivyo kuruhusu hatua zinazofuata za uwekezaji,
 2. Kuanza uchimbaji wa Makaa ya Mawe kupitia makampuni matano (5) ambayo yamepatikana mwaka wa fedha 2022/2023. Jumla ya tani 315,000 za Makaa ya Mawe zinatarajiwa kuchimbwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa Mradi wa Mchuchuma, na
 • Kulipia Ada ya Mwaka (Annual rent) kwa Leseni Ndogo za Uchimbaji nje ya leseni kubwa katika Mradi wa Makaa ya Mawe Mchuchuma. Baada ya malipo hayo, Kampuni zinaruhusiwa kuendelea na uchimbaji wa Makaa ya Mawe.
 • Utekelezaji wa Mradi wa Magadi Soda (Engaruka Soda Ash)

Ndugu Wanahabari,

5.5 Mradi wa Magadi Soda ulioko Monduli katika Mkoa wa Arusha pia ni mmoja ya Miradi ya Kielelezo Nchini. Katika kutambua umuhimu wa Mradi huo, Shirika limeendelea na hatua mbalimbali za utekelezaji ambapo:

 1. Shirika limefanikiwa kupata ofa ya Leseni moja (1) ya Uchimbaji badala ya Leseni 29 za awali, ambapo Dola za Marekani 121,950 kati ya Dola za Marekani 447,760 ya kodi ya mwaka (annual rent) zimelipwa.
 2.  Kuidhinishwa Vitabu vya fidia na Mthamini Mkuu wa Serikali (Chief Valuer) ambapo jumla ya Shilingi billion 14.5 zinatarajiwa kulipwa kwa wananchi kwa ajili ya fidia. Maombi ya fedha hizo tayari yamewasilishwa Wizara ya Fedha kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuweza kulipwa katika mwaka wa fedha 2023/2024.

5.6 Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linatarajia kufanya mambo yafuatayo katika kuhakikisha Mradi wa Magadi Soda unafikia katika hatua za utekelezaji:

 1. Kulipa Leseni za Uchimbaji ili kuruhusiwa kuendelea na hatua nyingine katika utekelezaji wa Mradi,
 2. Kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha Mradi (PAP) ili kuendelea na hatua nyingine ya utekelezaji wa Mradi, na
 • Kufanya mapitio/uhakiki wa taarifa zilipo kwenye tafiti zilizofanyika (Brine Resource appraisal and Techno-economic study review)
 • Mradi wa KMTC (Kilimanjaro Machine Tools)

5.7 Shirika limeendelea na mikakati mbalimbali ya kukifufua na kukiboresha Kiwanda cha kimkakati cha KMTC kilichoko Hai katika Mkoa wa Kilimanjaro. Maboresho mbalimbali yamefanyika na yanaendelea kufanyika yakijumuisha:-

 1. Kukamilika kwa manunuzi ya kemikali kwa ajili ya kutumika kwenye mtambo wa kuweka utando Chuma (Galvanizing Plant), manunuzi ya caustic soda, hydrochloric acid na zinc ammonium chloride,
 2. Kukamilisha manunuzi na usimikaji wa overhead crane kwa asilimia 100,
 • Kukamilisha ujenzi wa Tanuru la Kuyeyusha Chuma (Foundry),
 1. Kuendelea na ukarabati wa majengo ya Kiwanda ambapo hadi tarehe 30 Juni 2023 ukarabati umefikia asilimia 60,
 2. Kukamilika kwa Makubaliano ya awali kati ya NDC na UNCDF ili KMTC iingizwe kwenye Soko la Hisa,
 3. Kusaini mkataba/makubaliano na TEMDO wa kushirikiana kutengeneza vifaa tiba ambavyo vitapunguza gharama ya kuviagiza kutoka nje ya nchi,
 • Kukamilika kwa ukarabati wa mfumo wa umeme ambao utaongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Kiwanda cha KMTC na
 • Kuendelea na uzalishaji wa Mashine na Vipuri mbalimbali nchini.

5.8 Katika kuhakikisha kuwa Kiwanda cha KMTC kinaboresha mazingira yake ya uzalishaji pamoja na kufikia lengo lake, Shirika katika mwaka wa fedha 2023/2024 limepanga kufanya mambo yafuatayo: –

 1. Kufanya manunuzi ya fabrication machine kwa ajili ya uzalishaji wa Mashine na Vipuri, na
 2. Kufanya ukarabati wa mashine mbalimbali za Kiwanda ili kuendelea na uzalishaji na kuendelea na ukarabati wa majengo ya Kiwanda pamoja na kutafuta masoko sehemu mbalimbali kwa ajili ya bidhaa zinazozalishwa na Kiwanda.
 • Utekelezaji wa Miradi ya Makaa ya Mawe pamoja na Chuma

Ndugu Wanahabari,

5.9 Kwa kutambua umuhimu wa Makaa ya Mawe pamoja na Madini ya Chuma kwa ustawi wa Sekta ya Viwanda hapa nchini, Shirika limeendelea na hatua mbalimbali za kuhakikisha vitalu vya madini ya Makaa ya Mawe na Chuma inavyomiliki vinaanza uchimbaji wake mapema iwezekanavyo. Mpaka hivi sasa, NDC imefanikiwa kufanya yafuatayo: –

4.1 Mradi wa Makaa ya Mawe Katewaka

 1. Kukamilika kwa Mkataba wa Ubia (JV) na mwekezaji,
 2. Kukamilika kwa zoezi la utambuzi na uthaminishaji wa mali za wananchi wanaopisha Mradi ili waweze kulipwa fidia kabla ya zoezi la uchimbaji kuanza, na
 • Kuidhinishwa vitabu vya fidia na Mthamini Mkuu wa Serikali baada ya uthaminishaji kukamilika.

5.10 Aidha mipango ya Shirika kwa mwaka huu wa fedha katika utekelezaji wa Mradi huo ni kuhakikisha inakamilisha majadiliano na mwekezaji MMI Steel na kusaini Mkataba wa Ubia pamoja na kulipa Leseni za Uchimbaji ili kuendelea na hatua nyingine za utekelezaji ikiwemo uwekezaji.

4.2 Mradi wa Chuma Maganga Matitu

 1. Kukamilika kwa Mkataba wa Ubia (JV) na mwekezaji,
 2. Kukamilika kwa zoezi la utambuzi na uthaminishaji wa mali za wananchi wanaopisha Mradi ili waweze kulipwa fidia kabla ya zoezi la uchimbaji kuanza na
 • Kuidhinishwa vitabu vya fidia na Mthamini Mkuu wa Serikali baada ya uthaminishaji kukamilika.

5.11 Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 katika utekelezaji wa Mradi wa Maganga Matitu, Shirika limepanga kukamilisha majadiliano na mwekezaji na kusaini Mkataba wa Ubia (JV Agreement), Kulipa leseni za uchimbaji ili kuendelea akaay a nyingine za utekelezaji wa mradi.

         4.3 Mradi wa Makaa ya mawe ya Mhukuru

Ndugu Wanahabari,

5.12 Mradi huo upo Songea katika Mkoa wa Ruvuma ambapo katika utekelezaji wake tayari Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) wa kufanya utafiti wa kijiolojia (geological exploration) ulitiwa saini kati ya NDC na STAMICO tarehe 26 Septemba 2022. Katika mwaka wa fedha 2023/2024, Utafiti wa Kina wa Kijiolojia (detailed geological study) unatarajiwa kufanyika pamoja na kupata na kulipia Leseni ya Utafiti (Prospecting License).

 • Kongane za Viwanda – TAMCO-Kibaha, Nyanza, Kange na KMTC

Ndugu Wanahabari,

5.13 Shirika limeendelea na hatua mbalimbali za kuboresha Kongane za Viwanda inazozimiliki zilizoko katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa lengo la kuvutia uwekezaji :

 

 • Viwanda vya Hester Bioscience Africa; GF Assemblers; na Global Packaging Ltd vilivyopo chini ya TAMCO Industrial Park vimeendelea na uzalishaji pamoja na kuendelea kutanua wigo wa ajira nchini kwa kuajiri wananchi wanaozunguka maeneo ya Mradi,
 • Kiwanda cha GF Assemblers kilichopo TAMCO Industrial Park kimeanza ujenzi kwa kutanua eneo jipya la kuunganisha magari lenye ukubwa wa mita za mraba 21,970 ambapo kupitia Mradi huo kunatarajia kuongeza ajira kwa wananchi na kukuza uchumi nchini,
 • Kuanza ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuunganisha magari aina ya TATA katika eneo la TAMCO Industrial Park, Kibaha,
 • Kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Viuatilifu Road yenye urefu wa mita 230 kwa kiwango cha lami katika eneo la TAMCO Industrial Park,
 • Kutangaza eneo la TAMCO Industrial Park kwa wawekezaji wa nje ikiwemo katika Maonesho ya Dubai Expo pamoja na kuweka bango kubwa, na
 • Kwa upande wa Nyanza Industrial Park, kukamilika kwa ujenzi wa godown moja (1) mwezi Septemba 2022 pamoja na kumpata mzabuni wa kukarabati godown la pili ambapo ukamilikaji wa ujenzi huo utavutia wawekezaji.

5.14 Aidha, Shirika katika mwaka wa fedha 2023/2024, litahakikisha mazingira katika Kongane za viwanda yanaboreshwa ili kuvutia zaidi wawekezaji kwa kuhakikisha linafanya yafuatayo: –

 1. Kuendelea na ujenzi wa miundombinu katika Kongane za Viwanda ikiwemo barabara, ambapo ujenzi wa kipande cha barabara chenye urefu wa mita 320 ya China Boarder (katika TAMCO Industrial Park) kinatarajiwa kujengwa,
 2. Kuendelea na ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha magari aina ya TATA kilichopo Kongane la Viwanda TAMCO,
 • Kukamilisha ukarabati wa godown la pili Mradi wa Nyanza ili kuvutia wawekezaji katika Kongane la Nyanza, na
 1. Kuendelea na uzalishaji katika viwanda vilivyopo TAMCO Industrial Park pamoja na kutanua wigo wa ajira kupitia kuongezeka kwa uzalishaji baada ya uwekezaji wa eneo jipya kwa Kiwanda cha GF Assemblers.
 • Kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu (TBPL)

Ndugu wanahabari,

5.15 Katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutokomeza ugonjwa hatari wa Malaria, Shirika kupitia kampuni tanzu ya Tanzania Biolavides Product Limited (TBPL) inaendela na uzalishaji na uuzaji wa viuadudu. Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kilichoko Kibaha katika Mkoa wa Pwani kimefanikiwa kufanya yafuatayo:

 1. Jumla Lita 68,494 za Dawa za Viuadudu (Bactivec na Griselesf) zimezalishwa ambapo Lita 47,731.89 za viuadudu ziliuzwa ndani na nje ya nchi na kuingiza mapato ya jumla ya Shilingi 1,696,619,665,
 2. Kufanya vikao kazi na Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) kuhusu maendeleo ya Kiwanda katika kuongeza uzalishaiji, kuboresha utendaji na kuimarisha ustawi wa watumishi, na
 • Kupata Cheti cha Usajili cha Viuatilifu kinachoruhusu kuanza uzalishaji wa Viuatilifu (Bio-pesticides) kwa kipindi cha miaka mitano (5) mfululizo. Uzalishaji huo unategemea kuanza mwezi Septemba 2023.

5.16 Katika mwaka huu wa fedha 2023/2024, Shirika kwa kushirikiana na Kiwanda kimepanga kufanya mambo yafuatayo ili kuhakikisha lengo mahsusi la uanzishwaji wa kiwanda hicho hapa nchini linaweza kufikiwa:-

 1. Kufanya stadi ya uzalishaji wa mbolea za kibailojia (biofertilizer),
 2. Kutafuta masoko ya Viuatilifu vya kibailojia (biopesticides) na kuandaa mpango biashara,

iii.        Kusaini Mkataba wa Manunuzi wa Dawa za Viuadudu (Offtake Agreement) ili utekelezaji wake uweze kuanza, na

 1. Kuendelea na uzalishaji wa Viuadudu vya Kuangamiza Viluilui wa Mbu ili kuendelea kupunguza ugonjwa wa Malaria nchini.
 • Mashamba ya Mpira (Kalunga na Kihuhwi)

Ndugu Wanahabari,

5.17 Katika kusimamia kilimo cha mazao ya kimkakati ikiwemo Zao la Mpira, Shirika kupitia mashamba ya mpira inayoyamiliki yaliyoko Kalunga katika Mkoa wa Morogoro pamoja na Shamba la Kihuhwi lililoko Muheza katika Mkoa wa Tanga imefanikiwa kufanya yafuatayo: –

 1. Jumla ya Kilo 99,075 za mpira (rubber sheet) na Kilo 19,093 za Cuplum zilizalishwa hivyo kuwezesha uzalishaji wa malighafi za viwandani,
 2. Kupanda miche mipya 20,300 ya Mpira katika eneo la Hekta 45 katika shamba la mpira la Kalunga na Kihuhwi,
 • Kutayarisha miche mipya 81,237 katika shamba la mpira wa Kalunga, na
 1. Kutoa ajira za takribani watu 140 ambao wanahusika katika shughuli mbalimbali katika mashamba ya Mpira ya Kalunga,Mkoni Morogoro pamoja na Kihuhwi, Mkoani Tanga.

5.18 Aidha, Shirika katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 linapanga kufanya mambo yafuatayo ili kuhakikisha mashamba ya mpira yanaboreshwa pamoja na kuongeza thamani na tija ya Zao la Mpira:-

 1. Kuendelea na uzalishaji wa malighafi ya mpira ambayo imekua ikitumika katika viwanda katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali, na
 2. Kuendelea na upandaji wa miti mipya katika maeneo yaliyowazi ili kukuza uzalishaji wa zao hili kwa miaka ya usoni, pamoja na kuendelea kuimarisha miundombinu ya mashamba ya mpira ikiwemo matumizi bora ya zana za kisasa katika uzalishaji.
 1. DIRA NA MWELEKEO WA SHIRIKA KUENDANA NA MAZINGIRA YA SASA

Ndugu wanahabari,

6.1 Shirika hili ni Shirika mama na ni mkono wa Serikali wa uwekezaji ukilenga kuwezesha ushiriki wa wananchi katika kipindi cha muda wa kati na kirefu kumiliki uchumi wake na kuleta maendeleo ya Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Hivi, NDC inajielekeza katika kujijengea uwezo wa mtaji (fedha) na rasilimali watu kwa ajili ya uwekezaji wake ndani ya nchi ili hatimaye iwe na uwezo wa kushiriki katika uwekezaji nje ya nchi kutokana na rasilimali itakazozimiliki na kuziendesha kwa niaba ya Watanzania.

6.2 Aidha, Shirika kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara litajielekeza katika kutafuta suluhu za changamoto ambazo zimekuwa zikizorotesha uwezo na mwelekeo wake hususan changamoto za Kisheria na kisera; Kitaasisi na kimfumo; Miradi na kimikataba; Kimenejimenti; na Kifedha (mtaji na madeni).

6.3 Kwa upande wa Changamoto za kisheria na kisera, Shirika itajielekeza katika kufanya marekebisho au kutunga Sheria Mpya ambayo ni ya muda mrefu ili kwenda na mazingira ya sasa ya ushindani kibiashara. Mamlaka ya kutekeleza majukumu yake yanatokana tu na maagizo na utashi wa Serikali pasipo misingi ya kisheria.

6.4 Kwa upande wa Changamoto za kitaasisi na kimfumo NDC itakuwa na mwelekeo wa kuwa na msukumo wa kuwa taasisi ya kibiashara ambapo uendeshaji wake utafanywa katika mazingira ya ushindani na ushirikiano na sekta binafsi. Vilevile, Shirika litashughulikia changamoto ya mikataba na wabia ili kuhakikisha kuwa majadiliano ya kitaalam yanafanywa kwa tija na muda mfupi.

6.4 Kuhusu ukosefu wa miundombinu ya msingi na saidizi katika miradi ya kimkakati, Shirika kama mwekezaji mahiri, Shirika litajitahidi kuendeleza miundombinu yenye kujenga mazingira wezeshi ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuvutia wawekezaji mahiri kwenye ubia.

6.5 Shirika pia litaboresha uwezo wake wa kuandaa miradi inayokopesheka (Bankable projects) zitakazojumuisha tafiti za kiasi, ubora na aina ya madini. Hatua hiyo italiwezesha Shirika kuwa na msingi thabiti wa majadiliano na wabia hasa kwenye umiliki wa hisa.

6.6 Kwa upande wa changamoto za kimuundo na utendaji Shirika litaboresha mfumo wa uendeshaji wa Shirika unaozingatia pia uwajibikaji kwa kutofautisha umiliki na uendeshaji ili uendane na majukumu yake kwa mazingira ya sasa ya kiushindani na kibiashara. Shirika pamoja na kumilikiwa na Serikali litafanya uwekezaji na uendeshaji kama Sekta Binafsi kwa maana ya malengo, taratibu za ajira, manunuzi, uendeshaji na uwajibikaji. Kwenye shughuli zinazofanywa na NDC maamuzi ya haraka na ya uwazi ni muhimu sana kwa ufanisi wa Shirika.

6.7 Ili kuendana na mahitaji ya ujenzi wa ushindani, NDC inahitaji kujingea uwezo wa rasilimali watu ili kuwa na watumishi wenye utaalam na ujuzi unaohitajika. Uhaba wa wataalamu kwenye maeneo yanayohitaji ujuzi adimu yakiwemo wataalam wa uwekezaji, moduli za fedha na masoko. Shirika litakuwa na mfumo wa kuvutia watu wenye uwezo na vipaji kutoka taasisi za umma na Sekta Binafsi kutokana na uwezo wa kifedha na mfumo wa tuzo (reward system).

6.8 Kuhusu changamoto za kifedha (Mtaji na Madeni), Shirika litaendelee kutekeleza majukumu itakayopewa ya kusimamia miradi ya kimakakati kwa kushirikiana na wabia sambamba na uwekezaji wa mtaji.

Ndugu Wanahabari,

6.9 Mwelekeo wa mashirika mengi ya maendeleo duniani umekuwa ukibadilika kwa kufanyiwa maboresho kwa lengo la kuchangia maendeleo ya viwanda na kujengea nchi uwezo wa ushindani kwenye biashara na uwekezaji wa kimataifa. NDC siyo kisiwa, hivyo mabadiliko ya kimuundo na kiutendaji yanategemewa kuwa chachu muhimu ya kuongeza umuhimu wake katika uchumi wa nchi yetu. NDC bado ni chombo muhimu cha kutekeleza Dira ya Maendeleo. Kwa kuzingatia nafasi na umuhimu wa NDC katika Sera, Mipango na Mikakati ya Kitaifa pamoja na maslahi mapana ya Taifa, NDC mpya inapaswa kuendana na mazingira ya sasa na itakayokuwa chombo mama cha kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050. Hivyo NDC tunayoitaka ambayo ndiyo tunaijenga ni ile:

 • Itakayokuwa na uwezo wa kubainisha na kulinda rasilimali za kimkakati za Nchi;
 • Itakayosimamia na kuratibu miradi itakayojenga uwezo wa ndani wa uzalishaji na kuwezesha wananchi kumiliki hisa kwenye Miradi ya Kimkakati;
 • Itakayokuwa kiongozi katika kukuza maendeleo ya msingi ya miundombinu ya viwanda na ukuaji wake;
 • Itakayokuza rasilimali zitakazosaidia maendeleo ya uchumi kupitia viwanda na mambo mengine ya maendeleo;
 • Itakayoongoza uhamasishaji wa rasilimali kwa ajili ya kufanikisha na kufadhili maendeleo ya viwanda vipya na vilivyopo;
 • Itakayoishauri Serikali kisera na kimkakati katika kuanzisha, kuhuisha na kuendeleza viwanda na mambo mengine ya maendeleo; na
 • Itakayoshirikiana na wadau wengine katika huduma za tafiti na uelekezi katika ukuzaji na uendelezaji wa viwanda pamoja na mambo mengine ya maendeleo.

6.10 Mwelekeo wa NDC mpya ni ile inayoweza kulinda na kuendeleza rasilimali za kimkakati za nchi kwa niaba ya wananchi kwa kuzingatia mazingira ya sasa. Hivyo, muundo wa Shirika utaangaliwa upyaTutambue kuwa nchi zote duniani zina mashirika au taasisi ambazo zinaangalia maslahi ya kibiashara ya nchi hizo na sinasimamia mwelekeo wa kiuchumi wa Taifa.

6.11 Shirika linaandaa Sheria mpya ambayo itazingatia hali halisi ya mfumo wa uendeshaji uchumi nchini na mazingira ya uendeshaji wa Shirika na hitajio la kuifanya NDC kuwa chombo mahsusi cha Serikali cha kuchochea mabadiliko ya mfumo wa uchumi na biashara sawia na kusaidia maendeleo na kuwezesha uwekezaji. Sheria mpya na mfumo wa uendeshaji wa Shirika unaopendekezwa utazingatia haja ya kuweka mfumo rahisi wa kufikia maamuzi kuliwezesha Shirika kushirikiana na Sekta Binafsi na kutumia fursa za kibiashara zinazojitokeza. Aidha, Mpango Mkakati wa Shirika umehuishwa na umeainisha maeneo ya kimkakati ambayo Shirika litawekeza kwa kushirikiana na wawekezaji mahiri wa ndani na nje ya Nchi. Lengo ni kuifanya NDC kuwa Shirika ambalo lina nafasi kubwa ya kuchangia katika ujenzi wa Taifa letu kwa kushiriki moja kwa moja kwenye miradi ambayo ni ya kimkakati ikiwemo Mradi wa Mchuchuma na Liganga.

6.12 Kuna maeneo muhimu ambayo Sekta Binafsi inasita kuwekeza au inashindwa kuwekeza kutokana na sababu uwezo wa mtaji na teknolojia, muda mrefu wa kuanza kupata manufaa na sababu nyingine za kibiashara. Hivyo, kutokana na umuhimu wa maeneo kuwa na matokeo mapana kwa Taifa, Shirika linaweza kuwekeza ili kuvutia wawekezaji wengine au kuchochea manufaa ya muda mrefu na endelevu kwa Taifa. Vile vile, kuna maeneo ambayo Sekta Binafsi inaweza kuwa tayari kuwekeza lakini Serikali kwa namna moja au nyingine ina maslahi kwenye uwekezaji huo au sekta. Basi, Shirika linaweza kutumika kama mkono wa Serikali kuwekeza kwa kushirikiana na wadau wengine.

Ndugu wanahabari,

6.13 Ninapokaribia mwisho wa maongezi yangu, naomba kusema kwamba Shirika la Taifa la Maendeleo ni mkono wa Serikali wa uwekezaji na lina wajibu wa kuwekeza kwenye maeneo ya kimkakati kwa niaba ya Serikali kwa ajili ya maendeleo na maslahi mapana kwa Nchi. Ni Shirika ambalo lina jukumu la kuwezesha wananchi au Watanzania kumiliki viwanda na miradi mikubwa na kubadilisha mfumo wa uzalishaji ili kuwa na uchumi shindani. Kutokana na umuhimu wa Shirika na miradi inayoisimamia, hatua za kisera, kisheria na kimfumo zinahitajika kuendelea kuchukuliwa ili Shirika litekeleze majukumu yake kwa ufanisi kuendana na mazingira ya sasa.

6.14 Mwisho, niseme kuwa mafanikio ambayo NDC imeyapata yasingeweza kupatikana bila kuwa na timu inayoniunga mkono na kushikamana nami. Nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote wa Shirika la Taifa la Maendeleo kwa kazi ngumu wanayofanya kuhakikisha kwamba Shirika linarudi kwenye mstari.

6.15 Kwa namna ya pekee pia, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano anaotupa pamoja na Waziri wa Viwanda na Biashara na uongozi mzima wa Serikali kwa imani yao kubwa waliyonayo kwa Shirika.

6.16 Nimalizie kwa kurudia tena kuwashukuru ninyi wanahabari kwa kutenga muda wenu kuja kuungana nasi katika kuhabarisha umma wa Watanzania juu ya majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC). Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha taarifa zetu zinawafikia umma wa Watanzania ili kufikia malengo tuliyojiwekea ya kuwa uchumi wa kati na nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2025. Niwatakieni majukumu mema.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Mbariki Rais Wetu Mpendwa, Mungu libariki Shirika la NDC. Asanteni sana kwa kunisikiliza.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *