Wakulima wa Kijiji cha Kiloleni, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamepata matumaini mapya kufuatia hatua za haraka zilizochukuliwa na kiwanda cha viuadudu cha Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), kinachomilikiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), kudhibiti mlipuko wa minyoo weupe uliokuwa ukitishia usalama wa chakula katika eneo hilo.
Taarifa za awali za mlipuko huo ziliripotiwa tarehe 22 Februari 2026 kupitia vyombo vya habari, ambapo wakulima walieleza jinsi wadudu hao walivyoharibu mazao kwa kiwango kikubwa katika vijiji viwili. Walionya kuwa iwapo hatua za haraka zisingechukuliwa, hali ya njaa ingeweza kujitokeza kutokana na uharibifu wa mashamba.
Mara baada ya taarifa hizo kuripotiwa, TBPL ilichukua hatua za haraka kwa kutuma timu ya wataalamu wake kufanya tathmini ya kitaalamu na majaribio shambani. Baada ya kuwasili jijini Mbeya, wataalamu hao walikutana na wataalam kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Kanda ya Mbeya kwa ajili ya majadiliano ya kitaalamu kuhusu ukubwa wa tatizo na namna bora ya kulikabili. Tarehe 27 Februari 2026, timu ya pamoja ilitembelea vijiji vilivyoathirika na kubaini kuwa katika Kijiji cha Kiloleni kiwango cha uharibifu kilikuwa kikubwa kiuchumi na kilihitaji hatua za dharura.
Baada ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na tatizo hili wataalamu wa TBPL na TPHPA walijadili mkakati wa kitaifa wa udhibiti wa wadudu hao. Katika kikao hicho, ilielezwa kuwa tafiti zinaonesha minyoo weupe wanaweza kudhibitiwa kibiolojia kwa kutumia bakteria aina ya Bacillus thuringiensis, ambao husababisha kifo cha wadudu ndani ya kipindi cha wiki moja hadi tatu baada ya matumizi.
Katika kutekeleza hili maeneo mawili yalichaguliwa kwa ajili ya majaribio ambapo bidhaa za TBPL zilitumika kukabiliana na wadudu hawa dhurifu. Ili kuhakikisha uratibu mzuri wa zoezi hilo, TBPL na TPHPA waliunda kikosi kazi cha pamoja kitakachofanya kazi kama timu moja. Kikosi hicho kina jukumu la kusimamia matumizi ya viuatilifu vya kemikali katika maeneo teule kwa majaribio linganishi, kufuatilia maendeleo ya matumizi ya dawa kibaolojia za TBPL zilizotumika, kumuarifu Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuhusu hatua zilizochukuliwa, pamoja na kukutana na wanakijiji na kuwapa taarifa za kina kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali.
Tathmini ya awali inatarajiwa kufanyika baada ya siku saba tangu kuanza kwa majaribio, huku tathmini ya pili ikifanyika baada ya siku 21. Baada ya hapo, ripoti ya kina itawasilishwa katika Makao Makuu ya TPHPA kwa hatua zaidi.
Kitaalamu, minyoo weupe ni hatua ya lava ya mende, na hupitia hatua nne za ukuaji ambazo ni yai, lava, pupa na mende kamili. Katika hatua ya lava, wadudu hawa hulishwa mizizi ya mimea na mabaki ya viumbe hai ardhini, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa mazao. Wanaweza kuishi ardhini kwa muda wa hadi mwaka mmoja na kujifukia kina kirefu zaidi wakati wa baridi, jambo linalofanya udhibiti wake kuhitaji mbinu za kitaalamu na za muda mrefu.
TBPL itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wadudu hawa dhurifu wa mazao wanadhibitiwa. Hatua hiyo itakuwa mchango muhimu katika kulinda usalama wa chakula, kuimarisha kilimo endelevu na kuongeza tija kwa wakulima wa Mkoa wa Songwe na maeneo mengine nchini.
Kiwanda cha TBPL ni kiwanda kinachomilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja na ni cha kipekee barani Afrika na kinazalisha bidhaa za kibaiolojia za kupambana na Maralia, wadudu dhurifu wa mazao mbalimbali pamoja na mbolea za kibaolojia ambapo miongoni mwa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hiki ni pamoja na bidhaa za Thurisave 24, Bactivec, Griselesf, Dirmagon na Fosforina. Mkakati huu wa pamoja unalenga si tu kupunguza na kuangamiza minyoo weupe bali pia kuboresha afya ya mimea na kurejesha rutuba ya udongo uliokuwa umeathirika kutokana na mashambulizi ya wadudu hao.

