Ufufuaji wa KMTC wachochea kasi ya uchumi wa viwanda

Hatua ya Serikali kufufua na kuwekeza upya katika Kiwanda cha KMTC Manufacturing Limited kilichopo Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, imeanza kuzaa matunda baada ya kuimarisha uzalishaji wa mashine na vipuri vya viwandani, kupanua ajira na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ikiwa ni nguzo muhimu ya kujenga uchumi wa viwanda nchini.

Kiwanda hicho cha kimkakati, kilichoanzishwa miaka ya 1980 kwa ushirikiano wa Serikali za Tanzania na Bulgaria, kimepata uhai mpya baada ya kusimama uzalishaji tangu mwaka 1998.

Kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) na Wizara ya Viwanda na Biashara, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 5.1 katika kipindi cha miaka mitano, hatua iliyowezesha kurejesha uzalishaji, kusimika mitambo ya kisasa na kupanua wigo wa bidhaa.

Hayo yameshuhudiwa katika ziara ya Naibu waziri wa viwanda na biashara Dennis Londo alipotembelea kiwanda hicho Leo January 20,2026.

Akitoa taarifa ya kiwanda hicho, Meneja Mkuu KMTC, Leonard Mgoyo amesema kuwa baada ya kupokea fedha hizo, maboresho makubwa yamefanyika ikiwemo ujenzi wa tanuru la kuyeyushia chuma (foundry), usimikaji wa mtambo wa Hot Dip Galvanizing unaolinda bidhaa za chuma dhidi ya kutu hadi miaka 70, pamoja na ukarabati wa miundombinu ya umeme na majengo ya uzalishaji.

“Ufufuaji wa KMTC ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga msingi imara wa uchumi wa viwanda unaotegemea uwezo wa ndani”.

Amesema kiwanda sasa kina vitengo vinne vinavyofanya kazi ikiwemo karakana ya mashine, uundaji na uunganishaji wa vyuma, foundry na kitengo cha galvanizing ambavyo awali vingine havikuwepo.

“Kwa sasa, KMTC kinatoa ajira 174 zikiwemo 29 za moja kwa moja na 145 zisizo za moja kwa moja huku mpango mkakati wa kiwanda ni kutoa ajira za moja kwa moja 207 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 1,200 pindi uzalishaji utakapofikia uwezo wa juu”amesema.

Nae mkurugenzi Mkuu wa Shirika la maendeleo (NDC) Dr Nicholaus Shombe amesema ukuaji huo unatarajiwa kuchochea mnyororo wa thamani katika sekta za kilimo, madini, ujenzi, usafirishaji na mafunzo ya ufundi.

Amesema uwekezaji wa Serikali pia umewezesha KMTC kuanza kuhudumia taasisi na viwanda vikubwa vya ndani vikiwemo viwanda vya sukari vya TPC na Mkulazi, Tanzania Breweries Limited (Arusha na Mwanza), Harsho Group, GF Vehicles Assemblers, pamoja na mashirika ya Serikali kama TEMDO na Tanzania Sisal Board.

“Mazungumzo yanaendelea na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) ili kuhudumia viwanda vyake katika mikoa minne” amesema Dr Shombe na kuongeza;

“Mafanikio ya KMTC kuzalisha mashine na vipuri itapunguza mzigo wa uagizaji wa mashine na vipuri kutoka nje”amesema na kuongeza

“Takwimu zinaonesha Tanzania hutumia zaidi ya Shilingi trilioni 2.9 kwa mwaka kuagiza mashine na takribani Shilingi trilioni 2.5 kwa vipuri, bidhaa ambazo sehemu yake zinaweza kuzalishwa ndani kupitia KMTC kwa ubora na gharama nafuu”.

Shombe pia amesema Katika mikakati yao kiwanda kinaelekea kuanza uzalishaji wa grinding balls zinazotumika migodini, baada ya kubaini fursa kubwa ya soko hilo.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya kununua mtambo wa kuzalisha bidhaa hiyo, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi mchango wa KMTC katika sekta ya madini.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Londo ameipongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa hatua ya kuanza uzalishaji.

“Umuhimu wa kiwanda hiki tunafahamu, mbali na kuongeza ajira na kukuza uchumi wa viwanda lakini pia kuokoa fedha za serikali kuagiza mashine na vipuri itasaidia kuelekezwa fedha hizo katika miradi ya maendeleo, yote hii ikiwa na malengo ya kuchechemua uchumi wa nchi hii kufikia malengo ya dira ya taifa ya 2050”

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *