Wawakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP Tanzania, wakiongozwa na Mratibu wa Mipango, Bw. Amon Manyama, wamefanya ziara rasmi katika makao makuu ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) jijini Dar es Salaam. Katika ziara hiyo, Bw. Manyama alipokelewa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kujadili fursa za ushirikiano kati ya UNDP na NDC katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, hususan yale yanayohusisha kilimo, madini na uwekezaji katika maeneo yanayomilikiwa na NDC.
Dkt. Nicolaus Shombe alieleza kufurahishwa na ujio wa UNDP na kubainisha kuwa ushirikiano kati ya shirika hilo na sekta ya maendeleo ya viwanda ni muhimu katika kuimarisha na kuchochea uzalishaji bora. Aidha, alisisitiza dhamira ya NDC ya kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kufanikisha ajenda ya maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Bw. Amon Manyama alibainisha kuwa UNDP ipo tayari kushirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) katika maeneo ya uwekezaji kupitia wadau mbalimbali pamoja na eneo la kilimo, kupitia kampuni tanzu ya Tanzania Biotech Products Limited, hasa katika kusaidia upatikanaji wa viuatilifu hai kwa vikundi mbalimbali vya wakulima, ili kuleta mabadiliko chanya katika sekta hiyo.

