Wanawake wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) leo wametembelea Gereza la Wanawake Segerea, Ilala jijini Dar es Salaam na kukabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa mahabusu wanawake waliopo gerezani hapo. Msaada huo ulijumuisha sabuni, taulo za kike, sukari na mifagio ikiwa ni sehemu ya mchango wa NDC katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Machi 8, 2026.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya NDC, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake ya TUICO Tawi la NDC, Bi. Paula Kasange, alisema lengo la ziara hiyo ni kuonesha upendo, mshikamano na kuwafariji wanawake waliopo gerezani, akisisitiza kuwa bado ni sehemu muhimu ya jamii.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUICO NDC, Bi. Pulkeria Shao, alisema wamefarijika kuona baadhi ya mahabusu wanawake wakijishughulisha na kazi za mikono kama utengenezaji wa mabegi, jambo linaloonesha jitihada za kujifunza na kujipatia ujuzi utakaowasaidia baada ya kutoka gerezani.
Naye Mkuu wa Gereza la Wanawake Segerea, SSP Hamida Matimba, aliushukuru uongozi na wafanyakazi wa NDC kwa msaada huo, akisema umeleta faraja kubwa kwa wanawake waliopo gerezani na kuonesha upendo na mshikamano kwao.
Zoezi hilo ni sehemu ya utamaduni wa NDC wa kushiriki katika shughuli za kijamii na kusaidia makundi maalum yenye uhitaji katika jamii.

