WANANCHI 595 KULIPWA FIDIA MRADI WA MAGADI SODA ENGARUKA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amekutana na wananchi wa Engaruka katika zoezi la uhamasishaji kuelekea ulipaji wa fidia kwa wakazi wa maeneo ambapo Serikali inatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 14.4 kwa wananchi wanaotarajia kupisha utekelezaji wa mradi wa maendeleo wa Engaruka, Monduli-Arusha.

Dkt. Jafo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha fidia inalipwa kwa uwazi, haki, na kwa kuzingatia thamani halisi ya mali za wananchi. Katika mkutano huo, Waziri alibainisha mambo muhimu yafuatayo:

Wafidiwa Watalipwa Kwa Haki na Uwiano: Waziri alisisitiza kuwa Serikali imehakikisha kuwa jumla ya wafidiwa 595 watalipwa fidia kwa kiwango kinacholingana na tathmini iliyofanyika. Alieleza kuwa hakuna mwananchi atakayedhulumiwa au kupunjwa malipo.

Elimu Kuhusu Matumizi ya Fedha: Ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha za fidia, Serikali kwa kushirikiana na NDC na taasisi nyingine za kifedha kama UTT-AMIS, NEEC, NMB, na CRDB, imeandaa semina za kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo.

Faida za Mradi: Waziri alieleza kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ya Magadi Soda unaotarajiwa kuanza mara baada ya ulipaji fidia, utatoa ajira kwa wananchi wa eneo husika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

Dkt. Jafo alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Engaruka kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa bila changamoto. “Serikali iko nanyi, na dhamira yetu ni kuona kila mmoja wenu anapata haki yake. Tushirikiane kuhakikisha mafanikio ya pamoja,” alisisitiza.

Awali, akizungumza wakati wa mkutano huu wa hadhara, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, ambao ndio wataendesha zoezi la malipo haya ya fidia, amebainisha kuwa tayari NDC imejipanga vizuri kuelekea utekelezaji wa zoezi hilo ambalo linatarajia kuzinduliwa rasmi mwanzoni mwa mwezi Januari.

Jumla ya wanufaika 595 wanatarajiwa kulipwa na Serikali fidia ya jumla ya shilingi bilioni 14.4 kwa ajili ya kupisha utekelezaji wa mradi huu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *