Wanawake wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) wameungana na wanawake wengine kutoka taasisi mbalimbali kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika katika viwanja vya Mburahati Grounds jijini Dar es Salaam.
Katika maadhimisho hayo, mgeni rasmi alikuwa Albert John Chalamila, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye aliungana na mamia ya wanawake kusherehekea mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Wanawake wa NDC walitumia fursa hiyo kuonesha mshikamano wao na wanawake wengine, pamoja na kusisitiza umuhimu wa usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi, na nafasi ya mwanamke katika kuchangia maendeleo ya taifa. Kupitia ushiriki wao, walionesha dhamira ya taasisi hiyo katika kuunga mkono juhudi za serikali na wadau mbalimbali katika kuimarisha haki, fursa na ustawi wa wanawake.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Chalamila aliwapongeza wanawake kwa juhudi zao katika sekta mbalimbali za maendeleo, na kuhimiza jamii kuendelea kutoa nafasi sawa kwa wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi na maendeleo ya nchi. Aidha, alisisitiza umuhimu wa elimu, ubunifu na ushirikiano katika kuwainua wanawake na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia maendeleo yao.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 8 Machi, yakilenga kutambua mafanikio ya wanawake katika nyanja mbalimbali pamoja na kuhamasisha jamii kuendelea kupigania usawa wa kijinsia na haki za wanawake.
Ushiriki wa wanawake wa NDC katika maadhimisho hayo umeonesha dhamira ya taasisi hiyo kuendelea kushirikiana na jamii katika kukuza maendeleo jumuishi na kuhakikisha wanawake wanapata nafasi na fursa stahiki katika kujenga taifa imara.
