Waziri wa viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo ameutaka umma wa Watanzania kupuuzia taarifa zenye lengo la kupotosha ambazo zinaenezwa na watu wenye nia ovu juu ya utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa magadi soda ulioko Engaruka Mkoani Arusha.
Waziri Jafo ameyasema haya wakati akizindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi 592 ambao wanatarajia kupisha utekelezaji wa mradi huu ambapo kiasi cha shilingi bilioni 14.4 zimetengwa na serikali kwa ajili ya malipo ya fidia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi Waziri Jafo amesema hapo awali ulianza kutekelezwa katika eneo la ziwa Natron ambapo mwaka 2004 alipatikana mwekezaji, kampuni ya Tata Chemical Limited (TCL) ya India. NDC na TCL zilianzisha kampuni ya ubia iliyoitwa Lake Natron Resources Limited (LNRL) ambayo ilifanya tafiti mbalimbali zikiwemo upembuzi yakinifu na athari za mradi kwa mazingira (EIA). Mwaka 2006 katika warsha ya kujadili EIA wadau wa mazingira walipinga ujenzi wa kiwanda cha Magadi soda kwa kuwa eneo la Ziwa Natron ni mazalia pekee ya ndege aina ya Flamingo. Aidha, mkataba wa Ramsar ambao Tanzania ni wadau hauruhusu kufanyika kwa shughuli za maendeleo katika maeneo oevu, hivyo utekelezaji wa mradi ukakwama TCL iliamua kujitoa katika mradi huo mwaka 2006.
Jafo ameendelea kubainisha kuwa mara baada ya mradi huu kukwama mwaka 2008 serikali kupitia NDC kwa kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) liliamua kuanza upya kufanya utafiti mwingine wa awali katika eneo jingine la Bonde la Engaruka lililopo katika Wilaya ya Monduli, Mkoa wa Arusha umbali wa kiasi cha kilometa 60 kutoka ziwa Natroni. Hii ilifuatiwa na Utafiti wa kina (uchimbaji wa visima 16) uliofanyika mwaka 2010-2013 ambao ulionesha uwepo kwa magadi ya kutosha na kushauri ufanyike Upembuzi Yakinifu (Techno-economic Study) kwa ajili ya kujenga kiwanda na ndipo mradi huu ukaanza tena kutekelezwa.
Waziri Jafo ametumia fursa hii kuutaarifu umma kupuuza habari hizo kwa kuwa zina lengo la kupotosha na zimekuwa zikienezwa na watu ambao hawaitakii mema nchi yetu. Ukweli ni kwamba tayari NDC ambao ndio watekelezaji wa mradi huu wamekabidhiwa cheti cha Ithibati za mazingira kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kinachothibitisha kuwa uchimbaji wa magadi soda katika Eneo la Engaruka hauna athari zozote za kimazingira.
Awali akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Dkt. Nicolaus Shombe amesema kuwa NDC kama mtekelezaji wa mradi huo imetangaza na iko katika mchakato wa kumpata mwekezaji ambaye itashirikiana naye katika uchimbaji wa magadi huku akisisitiza kuwa mradi huo unaenda kubadilisha maisha kwa wakazi wa Engaruka pamoja na Taifa Kiujumla.
Akifafanua zaidi Dkt.Shombe amesema kuwa kulingana na upembuzi yakinifu uliofanyika ulikadiria kwa kiwango hicho cha mashapo, uzalishaji unaweza kuwa tani 1,000,000 kwa mwaka kwa zaidi ya miaka mia tano. Hali itakayopelekea kuliiingizia Taifa fedha za kigeni ambapo NDC imeamua kuwa kutakuwa na viwanda viwili vya kuchenjua Magadi ambavyo vitaendeshwa na wawekezaji wawili tofauti wenye uwezo kifedha, uzoefu na masoko.
Mradi wa Magadi soda wa Engaruka ni miongoni mwa miradi ya kimkakati ya Serikali ambapo utekelezaji wake utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda hapa nchini kwa kuwa hivi sasa Tanzania inalazimika kuagiza asilimia mia moja magadi soda kutoka nje ya nchi ambayo yanatumika katika viwanda mbalimbali.