Imeelezwa kwamba katika miaka minne ya Dkt Samia Suluhu Hassan Zaidi ya Bilioni 11.5 zimewekezwa katika kiwanda cha Tanzania Biotech Products ambacho kinatajwa kuwa na bidhaa bora zinazotumika ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania
Hayo yameelezwa leo na Katibu wa Wizara ya Vwanda na Biashara, Dkt Hashil Abdallah katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa sherehe za miaka 10 ya kiwanda hicho uliofanyika makao makuu ya kiwanda hicho kilichopo Kibaha, Mkoani Pwani.
Kwa upande wake Mfamasia mkuu wa serikali Ndg Daudi Msasi ameiomba ofisi za halmashauri kusimamia dawa zinazotengenezwa na kiwanda hicho kutumika ipasavyo kwa lengo la kutokomeza vimelea vya malaria.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Dkt Nicolaus Shombe amesema kwamba kiwanda hicho kimejengwa na Shirika la Taifa la Maendeleo Tanzania kwa niaba ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara.
Sambamba na hayo ameeleza kwamba zaidi ya billion 50 zimewekezwa katika ujenzi wa kiwanda hicho, na kudai kwamba wanasayansi wanaohudumu katika kiwanda hicho asilimia kubwa ni watanzania, pamoja na hayo kiwanda hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika kutafsiri sera na mipango ya Taifa la Tanzania.
Akitoa taarifa yake Mfamasia Mkuu wa Serikali Daudi Msasi ameiomba ofisi ya RAS kushirikiana kwa pamoja na halmashauri kusimamia matumizi ya dawa hizo kwa shabaha ya kuuwa wadudu pamoja na mbu kama jitihada zakutokomeza malaria kufikia mwaka 2030.
Akitoa salamu zake Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Raphael Morris amesema nchi nyingi za Africa zimenufaika zaidi na bidhaa zinazotengenezwa na kiwanda cha TBPL, ambapo pia ametumia mwanya huo kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania kwa mchango mkubwa uliyotokana na kuanzishwa kwa kiwanda hicho, pia ameitaka wizara ya kilimo kuhamasisha matumizi ya bidhaa za kiwanda hicho kwasababu ya ubora wake mkubwa.
Miongoni mwa nchi ambazo zimenufaika na dawa zinazotengenezwa na kiwanda hicho ni pamoja na Uganda, Kenya, Msumbiji, Angola, Botswana na Siri lanka.