Shamba la mpira la Kihuhwi lililopo Muheza mkoani Tanga ni kiungo muhimu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo magurudumu, gloves, viatu na vifaa vingine.
kwa kuona umuhimu huo, Afisa Biashara Mkoa wa Tanga, Afisa Biashara Wilaya ya Muheza na Afisa kilimo Wilaya ya Muheza wametembela shamba hilo linalo simamiwa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), kujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji shambani hapo.
“Wateja wetu ni wenye viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za mpira,” alieleza Charles Mjema, msimamizi wa shamba hilo na kuwataka maafisa hao kuwa mabalozi wazuri kuhakikisha wanalitangaza zao hilo lenye tija kubwa kwa Taifa.
Mjema aligusia kuwa shamba hilo limetoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania kwenye mnyororo mzima wa thamani na limeleta manufaa kwa kukuza pato la mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Nae msimamizi mwenza wa shamba hilo, Cyprian Pius alieleza NDC ina miliki shamba lingine la zao hilo mkoani Morogoro ambalo nalo huchangia kwenye ukuzaji wa uchumi.