MENU

KITILA MKUMBO AZINDUA ZOEZI LA ZOEZI LA KUANGAMIZA MBU JIMBO LA UBUNGO

Waziri wa Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amezindua rasmi zoezi la unyunyiziaji wa dawa za viuadudu vinavyozalishwa na kiwanda cha TBPL kilichoko Kibaha mkoani Pwani kwa ajili ya unyunyiziaji katika jimbo la uchaguzi la Ubungo ikiwa ni hatua ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kupambana na magonjwa yaenezwayo na mbu ikiwemo Malaria, Kikungunya pamoja na Dengue.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo ambalo limefanyika leo katika ofisi za CCM Manzese, Jijini Dar es Salaam, Prof. Mkumbo amesema unyunyiziaji huo unatarajiwa kuwa wa mfano kuwahi kufanyika hapa nchini na utafanyika kwa kuanzia katika kata ya Manzese na baadae katika jimbo lote la Ubungo huku akiwataka wananchi kuunga mkono zoezi hilo kwani kukamilika kwake kutasaidia kwa kiwango kikubwa cha kuboresha afya zao pamoja na kuondoa kabisa ugonjwa pamoja na vifo vitokananvyo na Malaria hapa nchini.

Prof. Mkumbo amebainisha kuwa kampeni hii itakuwa ni maalum kwa ajili ya jimbo zima la Ubungo ikiwa na lengo la kuifanya jimbo hilo la uchaguzi kuwa eneo salama lisilo na maambukizi wala vifo vitokananvyo na magonjwa yasababishwayo na mbu ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na ugonjwa wa Maleria.

Kwa upande wao wamiliki wa kiwanda cha Tanzania Biotech Product (TBPL) kiwanda kinachozalisha dawa hizo kilichoko Kibaha mkoani Pwani kupitia kwa Meneja wa Kiwanda hicho, Bw. Rafael Moya Rodriques amesema kuwa dawa zinazotengenezwa na kiwanda hicho ni dawa za kipekee na zinaondoa tatizo la uwepo wa mbu kwa asilimia mia moja na ni rafiki wa mazingira ikilinganishwa na dawa zingine ambazo matumizi yake hupelekea kutokea kwa athari kubwa kwa watumiaji pamoja na mazingira.

Bw. Rodriques ametoa ushuhuda wa matumizi ya dawa hizo katika nchi ya Cuba ambapo kabla ya matumizi ya dawa hizo Cuba ilikuwa na kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Maleria ambapo mara baada ya kuanza kuitumia kwa serikali kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wananchi suala la ugonjwa wa Malaria na magonjwa yatokanayo na mbu yametokomezwa kabisa nchini humo na yamekuwa ni historia.
Uzinduzi huo wa kampeni ya unyunyiziaji wa viuadudu katika jimbo la Ubungo umekwenda sambamba na utambulisho wa dawa mpya ya viuatilifu ya Thurisave 24 ambayo inatumika kuua wadudu dhurifu ambao wanaharibu mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na mbogamboga pamoja na matunda inayozalishwa pia na kiwanda cha TBPL.

Kiwanda cha TBPL kilichoko Kibaha mkoani Pwani ni kiwanda pekee ambacho kinazalisha dawa za Kibaiolojia hapa nchini na bara zima la Afrika ambapo kinamilikiwa na serikali kwa asilimia mia moja ambapo kwa hivi sasa kinazalisha dawa za viuadudu vya kuangamiza Malaria (Biolavicides) pamoja na dawa za kuua wadudu dhurifu wa mazao ya kilimo, mbogamboga pamoja na matunda.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *