MENU

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAKOSHWA NA KIWANDA CHA KUTENGENEZA VIPURI KMTC- MOSHI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo, Mifugo na Uvuvi ikiongozwa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mbunge wa Njombe mjini, Mhe. Deo Mwanyika wamepongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) katika kuhakikisha kuwa kiwanda cha KMTC kinaboreshwa na kuendelea na uzalishaji wa vipuri pamoja na mashine mbalimbali kama ilivyokusudiwa wakati wa uanzishaji wake.

Pongezi hizo zimetolewa na Mhe. Mwanyika mara baada ya kamati hiyo ya kudumu ya bunge kutembelea kiwandani hapo na kukagua shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kiwanda hicho kilichopo wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.

Mwanyika amesema kuwa KMTC ni kiwanda kikubwa cha kuzalisha viwanda vingine na kina mchango mkubwa kwenye uchumi huku akibainisha kuwa malighafi kubwa ya kiwanda hicho ni chuma kinachotumika kutengeneza vipuri na mashine na kama Taifa tukitaka tufikie malengo lazima tuanze u chimbaji wa chuma cha Liganga.

“Nimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuona umuhimu wa kiwanda hiki kwenye matumizi ya chuma, hivyo kuamua kutoa fedha za fidia kule Liganga ili chuma kile kitumike kiwandani hapa,” amesema Mhe. Mwanyika.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ameeleza kuwa wao kama Wizara yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya viwanda hapa nchini wanafurahi kuona kazi ya kuyeyusha chuma imeanza kiwandani hapo hivyo

kurejesha ajira kwa Watanzania ambao walikosa ajira kwa muda mrefu, huku akiishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha ujenzi wa tanuru la kuyeyusha chuma (foundry) pamoja na mtambo wa kutia utandu kwenye chuma (Galvanizing plant).

Ninamshukuru sana Mhe. Rais wetu kwa maono yake na kuyatekeleza maono hayo na amewathibitishia Watanzania kuwa Taifa letu litajengwa kwa uchumi wa viwanda hasa viwanda mama kama KMTC,” amesema Dkt. Kijaji.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Amir Mkalipa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, amewakaribisha wafanyabiashara mbalimbali kununua bidhaa zinazozalishwa na KMTC pia amewataka wenye viwanda kutohangaika kutafuta vipuri vya mitambo yao na kulazimika kuagiza nje ya nchi kwani KMTC wana uwezo wa kuchonga vipuri hivyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe ameeleza kuwa bidhaa zinazozalishwa na KMTC zinagusa sekta mbalimbali kama kilimo, viwanda, uchukuzi, usafirishaji, madini, misitu na ujenzi hivyo kuwa ni kiwanda chenye manufaa katika sekta hizo.

Licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa jitihada inazozifanya katika kukiendeleza kiwanda hicho Dkt. Shombe amebainisha kuwa Serikali imeendelea kufanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kiwanda hiki kinaboreshwa na hatimaye kiweze kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda nchini na kuinua maisha ya wananchi na kutoa ajira ambapo mpaka hivi sasa ujenzi wa tanuru la kuyeyusha chuma pamoja na mtambo wa kutia utandu kwenye chuma umeshakamilika.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *