MENU

TAARIFA KWA UMMA NDC YAWAVUTA WAWEKEZAJI KUTOKA CHINA KUWEKEZA NCHINI

Wawekezaji kutoka nchini China wakiongozwa na komrade Shen Dong, Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha nchini humo kutoka wilaya ya Zhonglou wamevutiwa na fursa za uwekezaji zilizopo Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) hasa kwenye sekta ya viwanda, madini na nishati na kuonesha nia ya kuja kuwekeza kwenye sekta hizo.

Komrade Shen Dong amesema hali ya kiuchumi na kisiasa imewavutia kuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji na kuona NDC ni mahala sahihi kushirikiana nao kwenye uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe, umeme jua (Solar power) na ujenzi wa viwanda.
Akiwa ameambatana na ujumbe wa wawekezaji kutoka China, komrade Shen Dong amesema amekuja na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali ili waone maeneo ya kuwekeza.

“Tumesikia habari zenu tukiwa China, tukaona tuje tujionee fursa zilizopo NDC ili tuwekeze,” amesema Komrade Shen Dong na kueleza kuwa miongoni mwa wawekezaji walioambatana nao wana nia ya kuwekeza kwenye umeme jua, madini, teknolojia ya viwandani, ujenzi wa makazi ya bei nafuu na usafirishaji.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Bw. Said Tunda, amesema NDC ni mahala sahihi kwa uwekezaji na hawana mipaka kwenye suala hilo hivyo milango ipo wazi.

“Sisi ni mkono wa Serikali katika uwekezaji na tunasimamia miradi kadhaa ikiwemo; Kiwanda cha kuzalisha mashine – KMTC cha mkoani Kilimanjaro, mradi wa makaa yamawe Mhukuru – Songea, mashamba ya mpira katika mikoa ya Tanga na Morogoro, na Kongane za viwanda zilizopo Kibaha, Tanga, Mwanza na Kilimanjaro ” amesema Tunda.

Aliendelea kueleza kuwa kiwanda cha Mang’ula kilichopo Morogoro ambacho kilijengwa na Wachina kwa ajili ya kuzalisha vipuri vya reli ya Tanzania – Zambia (TAZARA), kwa sasa kipo chini ya NDC, hivyo wanawakaribisha tena waje wawekeze ili kiwanda hicho kifufuke na kuleta tija kwa Taifa.

Pia aliwaeleza kuhusu kiwanda cha kuzalisha vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali, KMTC cha mkoani Kilimanjaro na kuwataka wachungulie fursa zilizopo hapo.

“KMTC ni kiwanda kikubwa chenye uwezo wa kuzalisha mashine mbalimbali, hii ni fursa kwenu na kwetu hivyo mnaweza kuangalia namna gani mnaweza kushirikiana na sisi kuendeleza kiwanda hicho chenye upekee wake nchini,” amesema Tunda.

Tunda alikazia kuwa Tanzania ina maeneo mengi yanayoweza kutumika kwenye uzalishaji wa umeme jua, hivyo wawekezaji hao wanakaribishwa kuwekeza kwani amefurahi kusikia miongoni mwa wawekezaji hao ana nia ya dhati ya kuwekeza kwenye nyanja hiyo.
Halikadhalika, Tunda hakusita kuwaeleza manufaa ya wao kuwekeza kwenye mradi wa makaa ya mawe wa Mhukuru uliopo Songea kwani ni miongoni mwa maeneo yenye mkaa bora ambao una soko zuri ndani na nje ya nchi hivyo ni fursa kwa wao kuwekeza.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *