MENU

LIGANGA, MCHUCHUMA MAMBO MSWANO

Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Watanzania  kuanza  kwa utekelezaji wa miradi mikubwa wa Liganga na Mchuchuma Wilayani Ludewa Mkoani Njombe baada ya kuanza ulipaji fidia kwa wananchi.

Akizungumza kwa njia ya simu na wananchi wakati wa hafla ya uzinduzi wa zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yenye madini hayo Mhe.Rais Samia amesema kuwa  lazima wananchi wote walipwe fidia pamoja na kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza ili miradi hiyo mikubwa ianze.

“Nataka niwaahidi fidia zote zitalipwa na kama kutakuwa wataalamu wamekosea,kuna watu wameachwa tutaliangalia lakini tunahakika tunalipa fidia ambayo tulishaifanyia kazi vizuri,ahadi yetu kwenu baada ya kulipa fidia mradi sasa  utaendelea,Mchuchuma na Liganga sasa utakwenda kuchangamka,ajira zitakwenda kupatikana,kodi kwa halmashauri zitakwenda kupatikana kutokana na mradi kuwepo,kwa hiyo niwaombe wananchi tushirikiane katika utekekezaji.Katika malipo kila mtu achukuwe anachostahiki halafu kwa vema tuje kushirikana kwenye mradi”alisema  Mhe Rais

Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji  ambae alikuwa Mgeni rasmi katika hafla hiyo ,amesema  kuwa Wizara sasa inaanza kwa kasi kubwa kutekeleza mradi wa madini hayo baada ya Serikali kuwalipa wananchi fedha zao.

“Sisi sasa kama watendaji ndani ya wizara hii tuko tayari kukimbia na wawekezaji ili mradi wetu huu uanze kutekelezwa,mradi huu wa Liganga na Mchuchuma ni mradi ambao unahistoria ndefu na ya muda mrefu ni mradi unaojumuisha uchimbaji wa chuma cha Liganga pamoja na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma ambapo kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Serikali mradi huu unaumuhimu mkubwa kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi yetu”alisema Dkt. Kijaji.

Alisema”Tumesikia kwa pamoja miaka 56 ijayo bado tutaendekea kunufaika na mradi huu,tunafahamu kabisa ni mradi wa kipekee zaidi duniani,hutoupata eneo lolote ndani ya ulimwengu huu zaidi ya Tanzania,na sifa yake moja kubwa tunazo rasilimali zote mbili zimewekwa kwa pamoja zinazotegemeana,tunayo makaa lakini tunacho chuma ambapo bila makaa, chuma huwezi kukiongeza thamani”alisema Waziri  Kijaji.

Nae Mkurugenzi mtendaji wa shirika la maendeleo la taifa NDC Dkt. Nicolaus Shombe amesema hadi jana usiku watu 39 walikuwa wameshalipwa fedha zao za fidia.

Ameongeza kuwa mradi huo unazaidi ya miaka 160 bila kutekelezwa na sasa umepata Rais ambae ameupa kipaumbele kati ya miradi inayotekelezwa nchini.

Mwaka 2013 Tafiti ya Makaa za Mawe pamoja na Chuma zilifanyika ,kwa kipindi hicho na  kugundua kwamba kuna tani milioni 428 za Makaa ya mawe katika eneo la ukubwa wa mraba 30 ambazo zinaweza kuchimbwa kwa miaka zaidi ya 140  na Chuma ambacho ni zaidi ya tani milioni 126 ambacho kinaweza kuchimbwa kwa miaka 58 “amesema Dkt.Shombe.

Aidha Mbunge wa Jimbo la Ludewa Mhe.Joseph Kamonga amesema licha ya wananchi wake kuanza kulipwa fidia Lakini bado wanatamani kusikia miradi ya madini hayo inaanza lini kwani wawekezaji wadogo wa mkoa wa Njombe nao wanataka vitalu vya madini.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe.Antony Mtaka amesisitiza wanufaika wa fidia hizo kuwa makini na kutofanya udanganyifu kutokana na malalamiko ya fidia za kipindi cha nyuma zilizofanywa na serikali.

Mtaka alisema kuwa uhakiki unaendelea kwa majina  77 kati ya 1,142 ambayo taarifa zake hazijakamilika.

Naye muwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Viwanda,Biashara Kilimo na Mifugo Mhe. Samweli Hhayuma,alisema kwamba Rais Samia amefanya miujiza kwa Taifa na litakwenda kusonga mbele.

Kwa sababu mradi huu ni mradi unaokwenda kubadilisha uchumi wa taifa letu,wananchi fikirieni tunaagiza chuma kutoka nje kwa kutumia bilioni moja kwa dola za kimarekani sasa hatutozitoa tena hizo,hivi viwanda vyote vya nondo,viwanda vya umeme,viwanda vya mabati, vitatumia chuma yetu,ujenzi wa reli” alisema Hhayuma.

Otimali Utulo ni mmoja wa wanufaika wa fidia ya kupisha mradi wa Liganga na Mchuchuma aalimshukuru Mhe.Rais Samia kwa kutimiza ahadi yake ya kulipa fidia licha ya kusubiri muda mrefu.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *