NDC NA SADC-DFRC KUJENGA USHIRIKIANO

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe,  amefanya mazungumzo na Bw. Stuart Kufen, Mkurugenzi Mtendaji wa SADC Development Finance Resources Centre (SADC-DFRC), jijini Dar es Salaam kujadili ushirikiano wa kimkakati baina ya NDC na SADC-DFRC katika nyanja ya uandaaji wa miradi na kuongeza ujuzi.

Kikao hicho pia kiliudhuriwa na Mkurugenzi wa Fedha wa NDC, Bi. Rhobi Sattima ambaye ndiye msimamizi wa mapato na matumizi ya NDC. Mkurugenzi wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe alimueleza Mkurugenzi wa SADC-DFRC miradi inayo simamiwa na NDC hasa dhamira ya NDC ya kukiendeleza kiwanda cha kuzalisha vipuri vya mashine na mitambo mbalimbali cha KMTC kilichopo mkoani Kilimanjaro.

“KMTC ni kiwanda cha kimkakati kwani kilianzishwa ili kuzalisha viwanda vingine kwa kutoa mashine katika viwanda hivyo,” alieleza Dkt. Shombe.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, akiwa kwenye picha ya pamoja na Bw. Stuart Kufen, Mkurugenzi Mtendaji wa SADC Development Finance Resources Centre (SADC-DFRC).

Aliendelea kueleza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kimefunga tanuru la kuyeyushia chuma ambalo litaongeza chachu ya uzalishaji kwa kuyeyusha chuma na kuzalisha bidhaa mbalimbali kiwandani hapo tofauti na zamani ambapo ilibidi watumie matanuru ya watu binafsi ambayo hayakuwa na ubora unaohitajika kimataifa.

Nae mkurugenzi Mkuu wa SADC-DFRC, Bw. Stuart Kufen alieleza dhamira yao ya kuendeleza mashirika ya kifedha na yenye miradi ya kimkakati kujikwamua kiuchumi na kuleta tija kwenye mataifa yao.

Alikazia kuwa SADC-DFRC inafanya kazi na Taasisi za Kifedha za Maendeleo  za nchi wanachama wa  Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).

Ikiwa na jukumu la kuanzisha na kuendeleza miradi kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, NDC itafaidika na ujuzi utakaotolewa na  SADC-DFRC katika nyanja ya uandaaji miradi kwani NDC inasimamia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini katika sekta mbalimbali kama madini, afya, uwekezaji na viwanda.

 Mkurugenzi wa Fedha wa NDC, Bi. Rhobi Sattima akiwa kwenye picha ya pamoja na Bw. Stuart Kufen, Mkurugenzi Mtendaji wa SADC Development Finance Resources Centre (SADC-DFRC).

Ujio wa SADC-DFRC ni jitihada za Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya taasisi hiyo yenye  Makao Makuu Bagorone, Botswana.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *