Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa Maendeleo (NDC)
Dkt. Nicolaus Shombe amekishauri Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), kuhakikisha
kinatengeneza mitaala ya kufundishia inayoendana na mazingira ya biashara yaliyopo
duniani hivi sasa.
Dkt. Shombe ameyasema haya jijini Dar es Salaam wakati
alipoalikwa kuwa mgeni rasmi katika shughuli ya CEO’s Breakfast tukio ambalo
liliwakutanisha wakuu wa Taasisi mbalimbali hapa nchini ambao kwa pamoja kwa
kushirikiana na chuo cha elimu ya biashara CBE wamejadili namna ya kukuza nguvu
kazi katika soko la ajira.
Akizungumza katika kongamano hilo Dkt. Shombe amesema mazingira ya hivi sasa ya ufanyaji wa biashara
yamebadilika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma hali inayoweza
kupelekea hata namna ya ufundishaji wa elimu ya biashara nayo kubadilika.
“Dunia ya leo mazingira ya biashara yamebadilika sana ni
tofauti na miaka iliyopita zamani ukiongelea bishara unaongelea Kariakoo lakini
saizi unavyoongelea biashara unaongelea ufanyaji wa biashara katika mitandao ya
kijamii unakuta mtu ana duka kubwa mtandaoni Instagram kuliko hata aliye na
duka mtaa wa Samora.” Alibainisha
Dk Shombe.
Dkt. Shombe aliitaka CBE kuhakikisha inakuja na
mitaala ambayo itakuwa inawaandaa wanafunzi wanaohitimu katika fani ya biashara
kuweza kutumia fursa zilizopo za kukua kwa sayansi na teknolojia na hatimaye
kuweza kushindana katika soko la ajira.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya
Biashara (CBE) Prof. Edda Lwoga amesema katika kuhakikisha wanazalisha wahitimu
wenye uwezo wa kupambana na soko la ajira mwaka 2022 chuo hicho kilifanya
utafiti maalum kwa lengo la kujua hali ya wahitimu wa chuo hicho na kuangalia
na jinsi wanavyoendana na hali halisi ya mahitaji ya soko la ajira.
Akiwasisha ripoti hiyo Profesa Lwoga amesema kuwa matokeo
ya uatafiti huo yameonyesha kuwa asilimia 79.5 ya wahitimu wa chuo hicho wanaweza
kujiajiri huku asilimia 59.5 ya wahitimu wameajiliwa na mashirika ya umma na
binafsi wakati asilimia 20 wamejiajiri na asilimia 20.5 bado wanatafuta ajira.
“Matokeo haya
yanaonyesha kuwa CBE tupo katika njia sahihi ya kuzalisha wataalam wanaohitajika
katika sekta ya viwanda na biashara lakini pia tunahitaji maboreho na hii CEO
Breakfast ni moja kati ya nia yetu ya kupata mrejesho ili tuweze kuboresha
elimu tunayotoa na kuzalisha wataalam wanaohitajika na soko” alisisitiza Prof Lwoga
Awali Mkuu wa Chuo cha CBE Mstaafu Prof. Emmanuel
Mjema ambaye pia ndiye mwanzilishi wa CEO’s Breakfast amewashukuru washiriki
walioshiriki katika tukio hilo na kwamba kufanikiwa kwake kunasaidia kwa
kiwango kikubwa kwa Chuo cha elimu ya biashara kuboresha huduma zake inazozozitoa
katika jamii kwa kuwa washiriki hupata muda wa kutoa maoni na mtazamo wao wa
uboreshaji wa huduma za chuo hicho.
CBE kilianzishwa mwaka 1965 ambapo kwa hivi sasa
inatoa elimu kwa ngazi mbalimbali ikiwemo shahada na uzamili katika fani mbalimbali
ambapo hii ni mara ya tatu kwa CEOs Breakfast kufanyika hapa nchini tangu kuanzishwa
kwake mwaka 2021 ambapo hutumika kama jukwaa la kuwakutanisha wadau wa kutoka
kada mbalimbali ambao kwa kushirikiana na CBE hujadili mambo mbalimbali
yahusuyo uboreshaji wa mazingira ya kufundishia elimu ya biashara hapa nchini.