Serikali imebainisha kuwa inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa miradi ya kimkakati iliyopo chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo nchini (NDC) inakwamuliwa kwa manufaa ya nchi pamoja na Taifa kiujumla.
Haya yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt.Hashil Abdallah katika kikao maalum baina yake na Katibu Mkuu Wizara ya Madini,pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya fedha ambao kwa pamoja walikutana ili kujadili namna ya kuondoka changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka Mkoani Arusha pamoja na mradi wa Uchimbaji wa chuma wa Liganga na Mchuchuma.
Awali akitoa taarifa kuhusiana na Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah amewaeleza makatibu wenzake kuwa NDC ni Shirika kubwa na ni nguzo muhimu kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi na kwamba katika jumla ya miradi ya kielelezo ya Kitaifa kumi na saba miradi miwili iko chini ya Shirika hilo ambayo ni mradi wa Magadi soda wa Engaruka pamoja na Mradi wa chuma cha Liganga na Mchuchuma.
“Mh. Katibu Mkuu, NDC ni mwekezaji kwa niaba ya serikali na limepewa dhamana kubwa na serikali na utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati itapelekea kuleta matokeo chanya katika kukuza uchumi wa nchi na ndio maana tumeamua tuwaite hapoa leo ili tujadili namna ya kuhakikisha tunasonga mbele na kutekeleza hii miradi” amebainisha Dkt. Abdallah.
Kwa upande wake Katibu mkuu wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya viwanda na Biasharakwa kumualika katika kikao hicho kwa kuwa amepata fursa ya kufahamu miradi mbalimbali inayotekelezwa na NDC na atahakikisha Wizara ya madini inatoa ushirikiano wa hali na mali kuhakikisha changamoto zinazokabili utekelezaji wa miradi hii zinakwamuliwa na utekelezaji unaanza mara moja kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC),Dkt.Nicolaus Shombe ameshukuru jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa miradi hii inafikia hatua ya utekelezaji ambapo amebainisha jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali ikiwemo ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao wanaotarajia kupisha utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma ambapo kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 14 za Kitanzania umekwishafanyika na sasa serikali iko mbioni kuhakikisha kuwa miundombinu na fidia zinalipwa kwa wananchi katika mradi wa Engaruka ili kuwezesha rasmi kuanza kwa utekelezaji wa hatua mbalimbali za kuelekea kuanza kwa mradi huo.
Kikao hiki kilikuwa kikao muhimu na cha kipekee ambacho kimefanyika Jijini Arusha katika Ukumbi wa Taasisi ya Usanifu wa Mitambo (TEMDO) kwa kuwakutanisha makatibu wakuu wa kisekta ambapo kwa pamoja wamejadili hatua mbalimbali zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma pamoja na kuweka mikakati ya kuhakikisha changamoto mbalimbali zilizopo katika utekelezaji wa miradi hii zinatatuliwa kwa kuhakikisha hatua mbalimbali za utekelezaji zinafanyika mara moja