Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) linaendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa mradi ya kimkakati ya Mchuchuma na Liganga, inayolenga kuongeza uzalishaji wa nishati na chuma nchini, kuchochea ukuaji wa viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za Tanzania.

Akizungumza Septemba 22, 2026 wakati wa kukutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji kutoka kampuni ya Shudao Investment Group Company Limited, wanaotarajiwa kutekeleza mradi huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema utekelezaji wa mradi unatarajiwa kuanza rasmi mwaka 2027.

Kwa mujibu wa Waziri Kapinga, mradi huo utatekelezwa kwa awamu sita, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma, ikifuatiwa na ujenzi wa mgodi wa chuma wa Liganga. Awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha makaa maalumu kwa ajili ya kuyeyusha chuma, huku awamu nyingine zikihusisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chuma, kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia mvuke unaozalishwa katika kiwanda cha chuma, pamoja na ujenzi wa barabara yenye urefu wa takribani kilomita 70 inayounganisha Mchuchuma na Liganga. Kupitia utekelezaji wa mradi hii, NDC inalenga kuwezesha Tanzania kutumia ipasavyo rasilimali zake za makaa ya mawe na chuma kwa ajili ya maendeleo ya viwanda, kuongeza uzalishaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za chuma na nishati kutoka nje.

Mradi wa Mchuchuma na Liganga ni miongoni mwa mradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa kupitia NDC na una umuhimu katika kujenga msingi wa uchumi unaotegemea uzalishaji, kuongeza fursa za ajira, kuibua viwanda vinavyotumia malighafi za ndani na kukuza minyororo ya thamani katika sekta ya madini na viwanda. Waziri Kapinga amesema utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kufikia azma ya Tanzania ya kujenga uchumi wenye thamani ya Dola za Marekani trilioni moja ifikapo mwaka 2050, sambamba na kuongeza uwezo wa nchi kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa ndani ya Tanzania.

Akizungumza kuhusu umuhimu wa mradi huo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, amesema Mchuchuma na Liganga ni miongoni mwa miradi ya kimkakati yenye uwezo wa kubadilisha kwa kiasi kikubwa sekta ya madini na viwanda nchini, kwa kuwezesha matumizi ya rasilimali za ndani katika uzalishaji wa chuma na nishati.

Dkt. Shombe amesema NDC itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wawekezaji katika kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa mradi huo yanafanyika kwa ufanisi, kwa kuzingatia malengo ya Taifa ya kuongeza uzalishaji, ajira, uwekezaji na thamani ya rasilimali za ndani.

“Mradi wa Mchuchuma na Liganga una nafasi muhimu katika kujenga uchumi unaotegemea uzalishaji wa ndani. Utekelezaji wake utafungua fursa za viwanda vipya, ajira na biashara, huku ukiongeza matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini,” amesema Dkt. Shombe.

Mradi wa Mchuchuma na Liganga unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya viwanda na kuongeza mchango wa rasilimali za madini katika uchumi wa Taifa.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *