Uongozi wa CITIC Metal Co. Ltd. kutoka China, ukiongozwa na Bw. Channing Wu, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Miradi Mipya katika Idara ya Uwekezaji wa Miradi, umetembelea Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa lengo la kufahamu miradi mbalimbali ya kimkakati inayosimamiwa na Shirika, hususan katika sekta ya madini.
Ujumbe huo ulipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, ambaye alieleza umuhimu wa ushirikiano na wawekezaji katika kuendeleza miradi ya kimkakati, kuongeza thamani ya rasilimali za Taifa na kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.
Katika ziara hiyo, uongozi wa CITIC Metal ulipewa maelezo kuhusu miradi ya uwekezaji inayosimamiwa na NDC pamoja na fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali ya kimkakati. Ziara hiyo imekuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mahusiano na kutengeneza fursa za ushirikiano wa uwekezaji kati ya Tanzania na wawekezaji kutoka China.
Aidha, Bw. Channing Wu ameonesha nia ya CITIC Metal Co. Ltd. kushirikiana na NDC katika miradi ya madini, hatua inayoweza kufungua fursa za uwekezaji na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika uendelezaji wa rasilimali za madini nchini.

