MENU

WAZIRI KIJAJI ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MIKATABA YA UCHIMBAJI MAKAA YA MAWE

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji ameshuhudia utiaji saini wa Mikataba ya Uchimbaji wa Makaa ya Mawe kwa wachimbaji wazawa katika Mradi wa mchuchuma baina ya Serikali kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) pamoja na Makampuni Matano ya wazawa yaliyoshinda zabuni hiyo, katika hafla ambayo imefanyika jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla hiyo Waziri Dkt. Kijaji ameonyeshwa kufurahishwa na hatua hiyo iliyofikiwa huku akisema utiaji saini huo ni wa kihistoria katika utekelezaji wa Miradi ya Liganga na Mchuchuma kwa kuwa ni kuendeleza maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuendeleza Sekta ya Viwanda nchini.

“Hii ni dhamira ya dhati na ya hali ya juu ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuhakikisha ndoto za utekelezaji wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma sasa zinatimia na rasilimali hizi ambazo zimekaa kwa muda mrefu bila kuwanufaisha wananchi ziwanufaishe na kuchangia katika uchumi wa Nchi,” amesema Dkt. Kijaji.

Waziri Kijaji ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchangia katika mafanikio hayo ambapo hapo awali alitidhia kutoa kiasi cha shilingi bilioni 14.4 za kitanzania ikiwa ni malipo ya fidia kwa wanufaika ambao watapitisha utekelezaji wa mradi huu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC Dkt. Nicolas Shombe amesema mchakato huo ulihusisha jumla ya Kampuni 25 ambapo jumla ya Kampuni 17 zilifanikiwa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya uchambuzi na ushindani na hatimaye zilipatikana Kampuni tano zilizokidhi vigezo, ambazo zimekodishwa vitalu katika Awamu ya kwanza ya Mradi huo.

Dkt. Shombe amebainisha kuwa Mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kiuchumi ikiwemo kutoa ajira zaidi ya 500 za moja kwa moja, kurahisisha upatikanaji wa nishati inayotokana na makaa ya mawe kwa Viwanda jambo litakalo chohea ukuaji wa Viwanda nchini pamoja na kuingiza Fedha za kigeni kwa mkaa utakao uzwa nje ya Nchi hususan Nchi jirani.

Jumla ya Kampuni tano zimetia saini makubaliano haya ya uchimbaji wa makaa ya mawe katika Mradi wa Mchuchuma ambazo ni Sheby Mix Investment Limited, Nipo Engineering Company Limited, Chusa Mining Company Limited, Kindaini Company Limited na Cleveland Mine and Service Company Limited, mikataba ambao itadumu kwa muda wa miaka mitano.

Naye Mwekezaji wa Kampuni ya Cleveland Mine and Service Company Limited Ndaisaba Ruhoro amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuwathamini wawekezaji wa kizawa na kuwapatia vitalu.

Amesema kwamba imani hiyo aliyowapatia wataitekeleza kwa vitendo kwa kuhakikisha wanafanya shughuli zao kwa uzalendo na umakini mkubwa kwa maslahi Mapana ya Nchi.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *