NDC na CRDB zaimarisha ushirikiano katika miradi ya kimkakati kuleta maendeleo nchini

Timu ya wataalam kutoka CRDB Bank Plc imetembelea Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimkakati katika kutekeleza miradi ya maendeleo nchini.

Kwa upande wake kiongozi wa timu ya CRDB Bank Plc, Dominick Timothy, ambaye ni Meneja Mwandamizi wa huduma za kibenki kwa Taasisi (Institutional Banking), alibainisha kuwa CRDB inaendelea kujikita katika kusaidia miradi ya kimkakati kupitia huduma za kifedha zenye tija.

Aliongeza kuwa benki hiyo ipo tayari kushirikiana na NDC katika kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati

Katika kikao hicho, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, alieleza umuhimu wa taasisi za kifedha kushirikiana kwa karibu na mashirika ya umma ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inapata rasilimali za kutosha. Alisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kukuza uchumi wa viwanda na kuharakisha maendeleo ya taifa.

Pande zote mbili zilieleza mafanikio ya ushirikiano wao wa awali, hususan katika zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya Liganga na Mchuchuma pamoja na mradi wa Maganga Matitu. Ushirikiano huo umechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha utekelezaji wa miradi hiyo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya madini na nishati.

Aidha, ziara hiyo ilitoa fursa kwa timu ya CRDB kujifunza kwa undani zaidi kuhusu miradi inayosimamiwa na NDC, hususan ile inayolenga kukuza sekta ya viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *