Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Shombe, amekutana na ujumbe kutoka kampuni ya Hong De Sheng ya nchini China kwa lengo la kujadili na kupata uelewa wa kina kuhusu miradi inayosimamiwa na shirika hilo hapa nchini. Mazungumzo hayo yamelenga zaidi sekta ya chuma ambayo ina nafasi kubwa katika kukuza uchumi wa viwanda.
Katika kikao hicho, pande zote mbili zimejadili fursa mbalimbali zilizopo ndani ya miradi ya chuma, ikiwemo uzalishaji, usindikaji na uongezaji thamani wa madini ya chuma. NDC imewasilisha mikakati yake ya kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa tija na kuleta manufaa kwa Watanzania.
Mwenyekiti wa kampuni ya Hong De Sheng, Bwana Lin Xiang Rong, ameonesha kuvutiwa na juhudi na mipango ya NDC katika kuendeleza sekta ya chuma. Ameeleza kuwa kampuni yake ina uzoefu mkubwa katika uwekezaji wa viwanda na iko tayari kushirikiana na Tanzania katika miradi hiyo.
Aidha, Bwana Rong ameonesha nia ya dhati ya kuanzisha kiwanda cha chuma hapa nchini, hatua ambayo itachangia kuongeza ajira, kukuza uchumi wa ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi.
Ugeni huu ni matokeo ya jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara chini ya Mhe. judith__kapinga , ambaye alifanya ziara nchini China mapema mwaka huu kwa lengo la kutafuta wawekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Kwa ujumla, hatua hii inaonesha mwelekeo chanya wa Tanzania katika kuvutia uwekezaji wa kimataifa, hasa katika sekta ya viwanda, na inaweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya uchumi wa nchi.

