Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera, amefanya ziara ya kikazi katika Makao Makuu ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kiteknolojia kati ya Tanzania na Cuba kupitia kampuni ya Tanzania Biotech Products Limited (TBPL), inayomilikiwa na NDC.
Katika ziara hiyo, Balozi Vera amesisitiza dhamira ya Serikali ya Cuba kuendelea kuiwezesha TBPL kwa kuleta teknolojia za kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Kitanzania ili kuwawezesha kutumia teknolojia hizo katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali za kibaiolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe, amemshukuru Balozi Vera kwa mchango na jitihada zake katika kuimarisha uhusiano wa Tanzania na Cuba, akieleza kuwa TBPL iko tayari kujifunza, kupokea na kutumia teknolojia zitakazoletwa.
Ameongeza kuwa NDC itaendelea kuimarisha ushirikiano na kampuni ya LABIOFAM ya nchini Cuba ili kuhakikisha TBPL inaendelea kukua kiteknolojia na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kibaiolojia zinazochangia maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.
Ushirikiano kati ya TBPL na LABIOFAM tayari umewezesha kuongezeka kwa bidhaa za kibaiolojia zinazozalishwa na kampuni hiyo, zikiwemo Thurisave 24 pamoja na mbolea hai za Fosforina na Dimargon, hatua inayodhihirisha matokeo ya ushirikiano huo katika kuendeleza teknolojia na uzalishaji wa ndani.

