NDC Yaimarisha Ushirikiano na Uongozi wa Wilaya ya Muheza kwa Maendeleo ya Shamba la Mpira Kihuhwi

Muheza, Tanga: Maafisa wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) wametembelea ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Muheza na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika usimamizi na maendeleo ya Shamba la Miti ya Mpira la Kihuhwi linalomilikiwa na NDC.

Shamba hilo lina ukubwa wa hekta 668.68, ambapo hekta 318 zimepandwa miti ya mpira. Pia, limekuwa likitoa fursa za ajira kwa wananchi wa vijiji vinavyolizunguka, hivyo kuchangia kukuza uchumi wa jamii.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Bi. Naima Chondo, amesisitiza umuhimu wa NDC kudumisha mahusiano mazuri na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuhakikisha uwekezaji huo unanufaisha jamii inayozunguka shamba hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mhe. Ayubu Sebabili, ameitaka NDC kuzingatia dhana ya Local Content kwa kutoa kipaumbele kwa wananchi wa eneo hilo katika fursa za ajira na shughuli nyingine za kiuchumi.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Viwanda vya Kuongeza Thamani wa NDC, Bi. Esther Mwaigomole, ameiomba Serikali kuboresha miundombinu ya barabara na upatikanaji wa umeme katika eneo hilo ili kurahisisha shughuli za shamba na kuongeza ufanisi wa mradi.

Kupitia ziara hiyo, NDC imeendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali za Mitaa pamoja na wananchi ili kuhakikisha miradi yake inaleta manufaa ya kiuchumi na kijamii.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *