MENU

UZALISHAJI WA BIDHAA ZA KIBAIOLOJIA KUONGEZEKA

Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa amesema Serikali ya Cuba itaendelea kutoa utaalam kwa kiwanda cha kuzalisha bidhaa za Kibaiolojia – Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) cha Kibaha – Pwani, ili kizalishe bidhaa nyingi za kibaiolojia mbali na uzalishaji wa viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu na viuatilifu vya kupambana na wadudu dhurifu vinavyo zalishwa kwa sasa.

Mhe. Mesa ametoa kauli hiyo leo tarehe 24 Januari 2024 alipotembelea Kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 23 hadi 25 Januari 2024.

Pia amesema kiwanda hicho kitaendelea kuwa mfano wa ushirikiano wa kihistoria uliopo baina ya Tanzania na Cuba katika sekta mbalimbali ikiwemo ya afya. “Nimepata bahati ya kukitembelea kiwanda hiki kwa mara ya pili sasa, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2016 wakati kinajengwa. Amesema Mhe. Mesa. Amesema kiwanda hicho kinatakiwa kutunzwa kwani ni chanzo cha ajira kwa watanzania lakini pia kinakuza uchumi wa Tanzania pamoja na kuimarisha afya za watanzania.

Awali akizungumza kumkaribisha Mhe. Mesa katika kiwanda hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhe. Abubakar Kunenge amesema kuwa anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhamasisha uwekezaji wa viwanda kwenye mkoa huo na kuwakaribisha wawekezaji zaidi kutoka Cuba kuja kuwekeza.

Miongoni mwa Viongozi wengine walioshiriki ziara ya Mhe. Mesa kwenye kiwanda hicho ni Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Mhe. Humphrey Polepole na Balozi wa Cuba nchini Tanzania, Mhe. Yordenis Despaigne Vera.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *