WAZIRI KAPINGA AIPONGEZA TBPL KWA UWEKEZAJI WA MBOLEA HAI, ATAKA KUONGEZA UZALISHAJI NA MASOKO

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameipongeza kampuni ya Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) kwa uwekezaji wake katika uzalishaji wa mbolea hai, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya rasilimali za ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano iliyofanyika katika kiwanda cha TBPL kilichopo Kibaha mkoani Pwani, Kapinga amesema uzalishaji wa mbolea hai nchini utapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza pembejeo hizo kutoka nje ya nchi huku ukiwawezesha wakulima kupata bidhaa bora kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Amesema ushirikiano uliowekwa kati ya TBPL, TFC na wadau wengine ni hatua muhimu katika kuimarisha minyororo ya thamani ya kilimo na viwanda pamoja na kukuza matumizi ya teknolojia na ubunifu katika sekta ya kilimo.

Kapinga ameeleza kuwa matumizi ya mbolea hai yana mchango mkubwa katika kurejesha rutuba ya udongo, kuongeza mavuno, kuboresha afya ya mimea na kupunguza athari za mazingira zinazotokana na matumizi ya mbolea za kemikali.

“Uzalishaji wa mbolea hai kupitia TBPL ni hatua muhimu katika kuongeza tija ya kilimo, kuchochea ukuaji wa viwanda vinavyotegemea malighafi za ndani na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa mbolea hai katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema.

Waziri huyo pia ameagiza menejimenti ya kiwanda hicho kuongeza uzalishaji na kuimarisha mikakati ya masoko ili kunufaika na mahitaji makubwa yaliyopo sokoni.

Amesema uwezo wa kiwanda hicho ni mkubwa na unapaswa kuendana na mikakati madhubuti ya masoko ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinawafikia wateja wengi zaidi na kuongeza ufanisi wa biashara.

“Lengo letu si kuzalisha pekee, bali kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinapata soko la uhakika na kiwanda kinaendelea kujiendesha kwa ufanisi wa kibiashara,” amesema.

Aidha, amezitaka taasisi zote zilizoingia makubaliano hayo kuhakikisha yanatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yenye manufaa kwa wakulima, sekta ya viwanda na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Kapinga pia amempongeza Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Dkt. Nicolaus Herman Shombe, kwa usimamizi wake wa miradi ya maendeleo na mchango wake katika kuendeleza shughuli za uzalishaji viwandani.

Katika hafla hiyo, Waziri Kapinga ameshuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano kati ya TBPL, TFC na wadau wengine kwa lengo la kuimarisha uzalishaji, usambazaji na matumizi ya mbolea hai nchini.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *