Wizara ya Viwanda na Biashara kukitengea kiwanda cha KMTC Manufacturing Limited Bilioni 5 ili kuongeza uwekezaji katika mashine za teknolojia ya kisasa.
Akizungumza kuhusu mpango huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe. Balozi Waziri Salum, amesema serikali imeona umuhimu wa kuboresha miundombinu ya uzalishaji kwa kuongeza mashine za kisasa ili kuongeza ufanisi na tija ya kiwanda hicho.
Amesema katika bajeti ya mwaka ujao, wizara itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya ununuzi wa mashine za kidijitali ambazo zitasaidia kuongeza kasi ya uzalishaji, huku zikichukua nafasi ya mashine za zamani zinazotegemea zaidi nguvu kazi ya mikono (manual).
Aidha, ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kukifanya Kiwanda cha KMTC kuwa kituo muhimu cha mafunzo kwa vijana kutoka Kilimanjaro, Arusha na mikoa ya jirani, ambapo watapata nafasi ya kujifunza ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira la sasa.
Serikali imebainisha kuwa kijana anayepata mafunzo kwa muda wa miaka miwili hadi mitatu ndani ya mazingira ya kiwanda anaweza kupata ujuzi wa kumwezesha kujiajiri au kuajiriwa kwa urahisi zaidi, hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana nchini.

